Friday, February 15, 2013

Uchambuzi Wa Habari: Kwa Hili La Simu, Anne Makinda Ameonewa…!


 

Ndugu zangu,
Kwenye vyombo vya habari juma hili, moja ya habari kubwa iliyochagizwa sana ni kitendo ch viongozi wa Chadema kutoa kwa wananchi, pale viwanja vya Mwembe Yanga, namba za simu ya mkononi ya Spika Anne Makinda na Naibu wake, Job Ngugai.

Kimsingi, viongozi wa Chadema waliofanya kitendo kile walikosea. Yawezekana kabisa kuwa madai ya Chadema kuwa Spika na Naibu wake wanaisiginya demokrasia ndani ya Bunge ni madai ya msingi, lakini, namna waliyochagua ya kufikisha madai hayo kwa wananchi haikuwa sahihi.
Ni kawaida, kwa baadhi ya viongozi wawapo majukwaani kusukumwa na jazba wanapoongea, lakini, hutokea pia, kauli za viongozi hao wawapo majukwaani zinapokosa umakini, kupelekea madhara makubwa.

Katika kazi yangu ya uandishi, nimeshawahi kutofautiana na Spika Makinda, si mara moja, mara ya mwisho ni kwenye hoja yake kuwa wabunge wawapo Dodoma wana maisha magumu, hivyo, kuhalalisha ongezeko la posho zao.

Lakini bado naamini, Spika Makinda ni binadamu kama wengine. Naye ni mzazi na mwenye familia yake inayomzunguka. Kitendo cha viongozi wa Chadema kutoa hadharani namba za Spika Makinda , za simu ya mkononi, kwenye umati wa watu wenye kero mbali mbali , na unaoambiwa kuwa watumie namba hizo kumpigia na kutuma ujumbe mfupi kwa Spika Makinda, bila shaka, kwa akili ya kawaida tu, kitapelekea Spika Makinda na mwenzake Ndugai kuwa na wakati mgumu. Maana, watu wale watakuwa wamechochewa.

Ikumbukwe, kijinsia Anne Makinda anaweza kuwa mhanga zaidi wa kupigiwa na kutumiwa jumbe za simu zenye hata kumdhalilisha kijinsia. Katika dunia hii kuna baadhi ya wanaume wenye maradhi ya kisaikolojia yenye kuhusihanisha masuala ya ngono. 

Kwamba kuna wanaume ambao hutafuta namba za simu za wanawake tu. Ikifika usiku, hupiga bila kuongea, wanachosubiri ni kusikia sauti ya mwananmke ikijibu na kisha kumaliza haja zao. Hao ni wagonjwa. 

Hivyo, unapotoa hadharani namba ya simu ya mkononi ya mwanamke, basi, unaweza pia kumuingiza katika hatari ya kupokea simu za ajabu ajabu kutoka kwa baadhi ya wanaume. Wako wapi wanaharakati wa haki za kibinadamu na kijinsia wa kumtetea Anne Makinda?
Tunajifunza nini?

Viongozi wa kisiasa wawe makini wawapo majukwaani. Mambo mengine wanaweza kuyafanya na hata kuyaongea majukwaani wakidhani kuwa wameyafanya kwa dhamira njema, lakini, matokeo yake yaweza kuwa na madhara makubwa.

Ingewezekana kabisa kwa viongozi wale wa Chadema kutoa hadharani namba maalum ya simu ya mkononi, ili watu wapige na watume jumbe fupi kwenye simu hiyo. Kisha, viongozi hao wangeweza kurekodi sauti zenye maoni ya watu yasiyo na matusi wala namna yoyote ya kudhalilisha. Wangekusanya pia jumbe hizo fupi kwa kuhariri zile zenye matusi na zenye kudhalilisha. Baadae zingewakilishwa kwa Spika Makinda na Naibu wake.

Ingewezekana pia kukusanya saini kutoka kwa wananchi zenye kuonyesha kuwa wanawapinga Spika na Naibu wake, na kwamba wanawashinikiza wang’oke. Hizi zote ni njia za kistaarabu kabisa za kuwasilisha malalamiko.

Tukishindwa kuonyesha mfano sasa, wa kufuata taratibu za kistaarabu, hatari yake tunaizoesha jamii kutumia njia za ovyo na nyingine zenye maovu katika kuwasilisha malalamiko yao. Na kesho huenda Spika wa Bunge atatoka Chadema.

Itakuwaje basi, pale kesho viongozi wa CCM nao watasimama Mwembe Yanga mbele ya wananchi wenye kero zao, na kutaja namba za simu ya mkononi za Spika wa Bunge linaloongozwa na Chadema?!

Hapana, hivi tunavyoenenda sivyo inavyopaswa twende. Na hakuna aliyekamilika. Tujisahihishe.
Maggid Mjengwa,

Iringa
0788 111 765

MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment