Jeshi la Polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni, limelalamikiwa kwa vitendo vya baadhi ya askari wake kuvamia vyumba vinavyodaiwa kupangwa na watu wanaodaiwa kuwa makahaba (madanguro) na kuwapora fedha, simu na vitu vingine vya thamani nyakati za usiku.
Aidha, askari hao wamedaiwa kuwageuza wanawake hao mashine za kutolea fedha (Atm) ambapo hufika katika vyumba vyao kila baada ya wiki moja na kuwadai fedha kati ya Sh.30,000 na 50,000 kila mmoja kama hongo ili wasiwafikishe polisi.
Malalamiko hayo yametolewa na baadhi ya akina mama wanaoishi eneo la Mwananyamala walipozungumza na NIPASHE baada ya askari hao kukamata wanawake zaidi ya 87.
Kiongozi wa wanawake hao, Judith Rugamwa alidai kuwa, askari hao kutoka vituo vya Oysterbay na Mabatini wamekuwa wakiwanyanyasa kwa kuwapiga, jambo ambalo ni kinyume cha haki zao binadamu.
"Wakitukamata huwa wanasema kosa letu ni kufanya ukahaba, lakini tukifikishwa kortini kosa linabadilika na kuwa uzembe na uzururaji, wakati wametukamata vyumbani kwetu ," alisema Judith.
Alisema wamechoka kunyanyaswa kama wakimbizi na kuonya kuwa sasa wanajiandaa kupambana na kila askari atakayefika hasa nyakati za usiku na kuwavunjia milango ya vyumba vyao ili kuwamata na kuwalazimisha wawape fedha huku wakimtaja afande Swai na Emma kuwa ndiyo wanaoongoza uovu huo.
Akizungumzia tuhuma hizo, afande Swai alijitetea kuwa yeye binafsi hajawahi kushiriki katika kuomba fedha wala kupora simu za wanawake hao licha ya kukiri kuwa ndiye anayeongoza misako yote Kinondoni.
"Kuhusu madai ya kuomba fedha, siwezi kukataa kwa sababu mimi huwa siingii vyumbani kukamata wanawake hao, badala yake askari wangu ndiyo wanaohusika moja kwa moja kabla ya kuwaleta katika gari ambayo huwa nawasubiri, lakini kama wanafanyiwa hivyo naomba wawataje kwa majina askari hao," alisema.
Kwa upande wake Kamanda wa polisi mkoani wa Kinondoni (RPC), Charles Kenyela, alisema amri ya kuwasaka na kuwakamata makahaba hao huwa inatolewa na ofisi yake na kwamba madai ya polisi wake kuchukua fedha na simu za watuhumiwa ni uongo mkubwa.
"Kama kuna mtu amewahi kufanyiwa hivyo aje ofisi kwangu na ushahidi ili ofisi yangu ichukue hatua kali za kinidhamu kwa sababu anayeshawishi, anayetoa na kupokea rushwa wote wanafanya makosa, waache kulalamika waje niwasilikize," alisema Kenyela.
No comments:
Post a Comment