Wednesday, May 29, 2013

NESI ANASWA KATIKA JARIBIO LA KUMTOA MIMBA MWANAFUNZI!


 
Mwanafunzi akiwa kitandani tayari kwa kutolewa mimba
MUUGUZI wa kike, Violet Shoo, mkazi wa jijini Dar ametiwa mbaroni na Jeshi la Polisi Kituo cha Buguruni, Ilala baada ya kunaswa katika jaribio la kutaka kumchoropoa ujauzito msichana mmoja aliyepandikizwa kama mwanafunzi kwa mtego makini ulioratibiwa na Oparesheni Fichua Maovu ‘OFM’
Tukio hilo lilitokea Jumamosi ya wiki iliyopita, saa 11 jioni kwenye zahanati iliyopo Tabata Matumbi, jijini Dar es Salaam.
 Nesi akidhibitiwa na polisi…
Muuguzi huyo alikutwa ndani ya zahanati hiyo akiwa na zana mbalimbali zinazodaiwa ni za kutolea mimba huku msichana huyo akiwa juu ya kitanda, tayari kwa kufanyiwa zoezi hilo haramu.
Awali, Ijumaa ya Mei 23, mwaka huu baadhi ya wakazi wa eneo hilo walitutumia ujumbe  wakimlalamikia muuguzi huyo kwamba amekubuhu katika matukio ya utoaji mimba hivyo wakaomba ikiwezekana OFM imuandalie mtego wa kumnasa ili kukomesha kitendo hicho.
“…huyu nesi amekuwa akiwatoa watoto wetu mimba, kwa siku anaweza kutoa hadi nne, sisi wazazi tumechoshwa, tunaomba mje. Anaitwa Violet…” ilisomeka sehemu ya meseji hiyo huku ikielekeza zahanati anapopatikana.
Nesi akiwa chini ya ulinzi….

Baada ya malalamiko hayo, kikosi cha upelelezi cha OFM chenye wasichana wawili kilikwenda kwenye zahanati hiyo na kukutana uso kwa uso na muuguzi huyo ambapo msichana mmoja aliomba kutolewa mimba na nesi huyo ambapo aliambiwa ni shilingi 50,000.
Kikosi kiliondoka kwa kumwambia muuguzi huyo kwamba wanafuata fedha mahali na wangerejea jioni wakiwa na  pesa mkononi.
Timu ya waandishi wetu wa habari  pamoja na Jeshi la Polisi waliweka mtego baada ya wakazi wa maeneo iliyopo zahanati hiyo kulalamika juu ya kukithiri vitendo vya utoaji mimba vinavyofanywa kwa muda mrefu na muuguzi huyo.
Wakazi wa maeneo hayo ambao hawakupenda majina yao yaandikwe , walidai kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi na kupiga simu katika chumba cha habari kuwa idadi kubwa ya wanawake wanatolewa mimba kwa siku katika zahanati hiyo bubu ambayo haina jina wala hadhi ya kutoa huduma.
Baada ya hapo, waandishi hao wa kike walirejea ofisini na kutoa taarifa kwa mabosi wao ambapo timu kamili ilipangwa.
Mkuu wa timu hiyo alianzia Kituo cha Polisi Buguruni ambapo alitoa taarifa kuhusu malalamiko ya wakazi wa eneo hilo na jinsi muuguzi huyo alivyofikia hatua ya kutaka alipwe elfu hamsini ili kukamilisha zoezi.
Afande mkuu akatoa maagizo kwa watu wa chini yake watatu, akiwemo askari wa kike mmoja kwa ajili ya kwenda kumnasa nesi huyo.
Msichana aliyepandikizwa kutolewa mimba akiwa na mwenzake walitangulia kufika kwenye zahanati hiyo lakini hawakumkuta muuguzi huyo.
Mfanyakazi mmoja wa zahanati hiyo alimweleza ‘mtolewa mimba’ kwamba nesi huyo alikwenda kusuka na tayari ameshawasiliana naye hivyo wasubiri.
Saa kumi na nusu, muuguzi huyo aliwasili kwa ajili ya kazi hiyo huku mawasiliano yakifanyika kati ya mtolewa mimba na waandishi waliokuwa jirani na eneo la tukio.
Ndani ya dakika kumi, waandishi na polisi waliitwa eneo la tukio wakijulishwa kwamba ‘mjamzito’ huyo ameshavua nguo tayari kwa kazi ya kuchoropolewa mimba.
Kikosi kazi kilivamia zahanati hiyo ambapo walikuta zoezi linaendelea. Polisi wenye ujuzi wa kazi za kunasa matukio walimtia mbaroni muuguzi huyo akiwa na zana za shughuli huku wakimwambia kosa lake.
 
Vifaa vilivyotumika….
Wakati huo, mjamzito alikuwa yupo kitandani katika maandalizi ya kutolewa mimba.
Wananchi waliokuwepo eneo la tukio wakati mtanange ukiendelea, walionekana kufurahishwa na kitendo cha kukamatwa kwa muuguzi huyo huku wakidai walikuwa wamechoka naye kutokana na vitendo vyake vya kutoa mimba hadi kwa wanafunzi.
“Tumekuwa tukijitahidi kutoa taarifa katika vyombo vya dola ikiwemo ofisi ya mwenyekiti wa serikali ya mtaa wetu lakini hakuna hatua zozote zilizokuwa zikichukuliwa, ndiyo maana tukaamua kuwasiliana na nyie waandishi wa habari ili mtusaidie,’’ alisema mkazi mmoja bila kutaja jina lake.
Muuguzi huyo alipoulizwa kwa nini amekuwa akijihusisha na vitendo hivyo, alikaa kimya.
Mjumbe wa Nyumba Kumi, Shina Namba 26, Tawi la Mandela, Rogasian Chadima alikuwepo katika eneo la tukio baada ya kufuatwa na polisi, naye aliahidi kufuatilia suala hilo akisema kwanza hakujua kama kuna zahanati katika eneo lake.
Safari ya kwenda polisi kwa mahojiano ilianza hapo huku muuguzi huyo akiwa na ‘ushahidi’ wake mkononi. Muda mwingi alionekana asiyeamini macho yake kwa kile kilichomtokea.
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment