Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bw. Ban Ki-Moon ameitaka serikali ya Rais Bashar al-Assad wa Syria kukubali kufanya mazungumzo ya amani na upinzani, saa chache baada ya Assad kuahidi kuendelea na mapigano.

Bw. Ban ametoa kauli hiyo kwa kuzingatia tamko lililotolewa na kiongozi wa upinzani wa muungano wa kitaifa Ahmed Moaz al-Khatib, akisema hiyo ni fursa ambayo haipaswi kupotea.
Mapema jana, Rais Assad alisema hatopiga magoti kwa shinikizo linaloongezeka na jaribio la mapinduzi. 

Aidha, Ban amesema umoja huo unapaswa kuhakikisha unatumia azimio la kidiplomasia kutatua mzozo wa Syria na siyo kufanya uvamizi wa kijeshi. 

Wakati huo huo, watu 13 wamekufa na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya bomu la kutegwa kwenye gari kulipuka kwenye mpaka wa Uturuki na Syria.
Wizara ya mambo ya ndani ya Uturuki imesema raia watatu wa Uturuki ni miongoni mwa waliouawa.