Thursday, July 26, 2012

MH: MKAPA AMEASA JAMII ZA KIAFRIKA ZIHAMASISHWE KUHUSU TOHARA YA HIARI KWA WANAUME.


Mhe. Benjamin Mkapa akiwasili hotelini tarehe 21 Julai 2012, kuhudhuria Kongamano la XIX la Kimataifa la UKIMWI linalofanyika Mjini Washington D.C. Kushoto ni Balozi wa Tanzania Marekani Mhe. Mwanaidi Sinare Maajar. 
Mhe. Benjamin Mkapa akisalimiana na Dr. Ellen Mkondya-Senkoro, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS mara baada ya kuwasili hotelini tarehe 21 Julai 2012, kuhudhuria Kongamano la XIX la Kimataifa la UKIMWI linalofanyika Mjini Washington D.C.
Mhe. Benjamin Mkapa akipewa taarifa na Mhe. Mwanaidi Sinare Maajar, Balozi wa Tanzania nchini Marekani mara baada ya kuwasili Washington D.C kuhudhuria Kongamano la XIX la Kimataifa la UKIMWI kuanzia Julai 22-28, 2012. Wengine kwenye picha ni Dr. Ellen Mkondya-Senkoro, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa HIV/AIDS na picha nyingine ni Ms. Eileen A. Swai, Msaidizi wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa. 
Mhe. Benjamin Mkapa akiwasili kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Washington Convention Centre Julai 23, 2012 kuhudhuria Kongamano la XIX la Kimataifa la UKIMWI linalofanyika Mjini Washington D.C. 
Ma-Champion wa HIV Free-Generation Rais Mstaafu wa Tanzania Mhe. Benjamin Mkapa na Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe. Joachim Chisano wakifuatilia mojawapo ya mikutano ya Kongamano la UKIMWI kwenye Ukumbi wa Mikutano wa mjini Washington. Pembeni ni Mhe. Mwanaidi SinareMaajar, Balozi wa Tanzania Marekani na Dr. Ellen Senkoro wa Taasisi ya Benjamin Mkapa.
Pichani Juu na Chini ni Ma-Champion wa HIV Free-Generation Rais Mstaafu wa Tanzania Mhe. Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Msumbiji Mhe. Joachim Chisano na Rais Mstaafu wa Zambia Mhe. Kenneth Kaunda wakijiandaa kabla ya mjadala kuanza kwenye mojawapo ya mikutano ya Kongamano la UKIMWI kwenye Ukumbi wa Mikutano wa mjini Washington D.C. 
Rais Mstaafu wa Tanzania Mhe. Benjamin Mkapa akihitimisha mjadala kuhusu Mpango wa Tohara ya Hiari kwa Wanaume ili kupunguza maambukizi ya UKIMWI kwenye mojawapo ya mikutano ya Kongamano la UKIMWI kwenye Ukumbi wa Mikutano wa mjini Washington D.C.
Washington DC;Mhe. Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewaasa viongozi wa Nchi za Kiafrika kuchukua hatua ya kuhamasisha jamii za kiafrika kuhusu mpango wa tohara ya hiari kwa wanaume (Voluntary Medical Male Circumcision for HIV Prevention) kama mojawapo ya njia ya kupunguza maambukizi ya UKIMWI barani Afrika.
Mheshimiwa Mkapa aliyasema hayo alipokuwa anahitimisha mojawapo ya mijadala ya pembeni (Satelite Session) iliyokuwa inaendelea wakati wa Kongamano la XIX la Kimataifa la UKIMWI linaloendelea Mjini Washington DC, Marekani ambapo watu takribani 22,000 wanahudhuria. Mjadala huo uliovutia mamia ya wajumbe hususan kutoka Afrika kuhusu tohara ya hiari kwa wanaume, uliendeshwa na Bi. Brenda Wilson kutoka Afrika  Kusini ulielezea tafiti za kisayansi kuhusu mpango huo kama njia ya kupunguza maambukizi ya UKIMWI.
Rais Mkapa alisema mpango huu ni muhimu kutekelezwa na viongozi wa nchi za Kiafrika kwani imethibitishwa na tafiti zilizofanyika kwa Waafrika kwamba unapunguza maambukizi kwa asilimia 60, ambapo alisema si jambo dogo katika harakati za kutokomeza UKIMWI. Aliongeza kuwa ni mpango uliopendekezwa na sisi Waafrika wenyewe na ni wa hiari na hivyo hakuna atakayeshurutishwa.
 “Umebuniwa na nchi za magharibi, lakini umetafitiwa na kuthibishwa na sisi Waafrika wenyewe, hivyo ni mpango wetu huu” alisisitiza Rais Mkapa huku akishangiliwa kwa makofi na wajumbe wa mjadala huo.
Ili kutekeleza mpango huu wa tohara ya hiari kwa mafanikio, Mhe. Mkapa alielekeza mambo matatu. Kwanza nchi za kiafrika inabidi zitengeneze sera na mikakati madhubuti ya jinsi ya kukabiliana na janga hili la UKIMWI. Pili mipango na mikakati hiyo imilikiwe na wananchi wa nchi husika ili wao wenyewe wathibitishe ushiriki wao na sio kuonekana kama shuruti .Na mwisho mipango na sera za kukabiliana na UKIMWI itekelezwe kwenye mazingira ya ukweli na uwazi ili jamii za kiafrika ziweze kutambua athari za janga hili la UKIMWI.  Pia serikali nazo zitenge fedha za kusaidia katika mapambano haya na si kutegemea fedha za wafadhili tu.
“Umefika wakati sasa dunia nzima ielekeze nguvu zake kwenye kutokomeza ugonjwa huu hatari ambao unaua maelfu ya watu kila siku” Alisema Mhe. Mkapa na kuongeza kuwa mataifa mbalimbali duniani hutoa misaada haraka sana mara majanga ya dharura yanapotokea,  kama vile mafuriko, ajali n.k. Lakini janga la UKIMWI ni kama dharura  inayoendelea na sasa ni wakati muafaka dunia nzima itazame janga la UKIMWI kama dharura na inayoendelea.
Naye Mwenyekiti mwenza wa Mpango wa Tohara ya Hiari wa PEPFAR Dkt. Emmanuel Njeuhmeli alithibitisha tafiti hizo kwa kutoa mfano wa Zimbabwe ambapo maambukizi ya UKIMWI yanakadiriwa kupungua kwa asilimia 45 ndani ya kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mpango huo.
Wengine walioongea katika mjadala huo ni Angelo Kaggwa (Uganda), Mhe. Dkt. Speciosa Wandira (Uganda), Bi. Henrica Okondo (Kenya), Chifu Jonathan Mumena (Zambia), Mhe. Oburu Oginga (Kenya), Mhe. Dkt. Christine Ondoa (Uganda), na Mhe. Blessing Chebundo (Zimbabwe). Mjadala huo pia ulihudhuriwa na marais wastaafu wanaojishughulisha na mapambano dhidi ya Ukimwi  ( wajulikanao kama Champions for AIDS Free Generation)Mhe. Joachim Chisano, Rais Mstaafu wa Msumbiji na Mhe. Kenneth Kaunda, Rais Mstaafu wa Zambia
Mhe. Mkapa amehudhuria Kongamano hili kubwa la UKIMWI kwa mwaliko wa taasisi ya Champions for HIV-Free Generation inayoongozwa na Rais Mstaafu wa Botswana Mhe. Festus Moghae, ambapo Mhe. Mkapa ni mmoja wa Ma-Champion nane wa taasisi hiyo.
Kongamano la XIX la Kimataifa la UKIMWI limeanza Washington DC tarehe 22 Julai hadi 28 Julai 2012 ambapo watu mashuhuri na viongozi mbalimbali wa Marekani wamehudhuria akiwemo Rais wa Marekani Mhe. Barack Obama.  


Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania Marekani
Julai 25, 2012
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment