Wednesday, October 10, 2012

MKURUGENZI MKUU WA MSD ASIMAMISHWA KAZI.


 
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi akitoa ufafanuzi  kwa waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali kufuatia kubainika kwa matumizi ya dawa bandia za kupunguza makali ya Ukimwi zenye jina la Biashara TT –VIR 30.
Mmoja wa maafisa kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwenye vyombo vya habari akiwaonyesha waandishi wa habari Dawa badia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVS) zilizoondolewa katika vituo vya kutolea huduma mara baada ya kugundulika.
Makopo ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi yakitofautiana vifungashio. Kopo la kwanza kushoto linaonyesha dawa halisi  ya kupunguza makali ya Ukimwi iliyokidhi viwango ikifuatiwa na makopo 3 yenye dawa bandia ya kupunguza makali ya Ukimwi yenye jina la biashara TT –VR 30 toleo namba 0c.01.85  yaliyotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd.(Picha na Aron Msigwa – MAELEZO).

Na. Aron Msigwa –MAELEZO.

Serikali imewasimamisha kazi mkurugenzi mkuu wa Bohari ya Dawa nchini (MSD) ,Mkuu wa kitengo cha Udhibiti na Ubora na Afisa Udhibiti Ubora wa ohari hiyo ili kupisha uchunguzi dhidi yao kufuatia kuruhusu kusambazwa kwa dawa bandia za kupunguza makali ya UKIMWI aina ya TT –VIR 30 katika vituo  mbalimbali vya kutolea huduma  za afya nchini.

Aidha imepiga marufuku usambazaji na matumizi ya dawa aina ya TT –VIR 30 toleo na 0C .01.85 inayotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) kufuatia dawa hiyo kutengenezwa chini ya kiwango na kutofaa kwa matumizi ya binadamu.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hussein Mwinyi amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa mara baada ya kubaini kuwepo kwa dawa bandia ya kupunguza makali ya Ukimwi katika hospitali ya wilaya ya Tarime kufuatia ukaguzi uliofanywa na Wizara ya Afya kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA).

Amesema kuwa ukaguzi na uchunguzi wa kimaabara dhidi ya dawa hiyo isiyokidhi viwango ulibainia kuwa nyaraka zilizopo kuhusiana na dawa hizo unaonyesha kuwa Kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd (TPI) waliiuzia Bohari ya Dawa (MSD) dawa hiyo bandia toleo namba 0C. 01. 85  iliyotengenezwa nchini mwezi Machi 2011 na kuonyesha mwisho wa matumizi yake mwezi Februari 2013.

Amefafanua  kuwa dawa hiyo bandia ilikua na dawa zenye rangi mbili tofauti njano na nyeupe na kuwa na viambata tofauti vilivyopaswa kuwepo aina ya Efaverenz badala ya Niverapine, Lamivudine na Stavudine na kuongeza kuwa vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika vilikua tofauti na vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA.

Dkt. Mwinyi amesema kuwa serikali inahakikisha kuwa dawa zenye ubora unaotakiwa za kupunguza makali ya UKIMWI zinaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma kote nchini na kuwaagiza waganga wakuu wa mikoa, wilaya  na kamati za dawa na Tiba katika vituo vya huduma za afya kuhakikisha kuwa zinapokea, kuhakiki na kusimamia kikamilifu ubora na matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba nchini.

Kuhusu upatikanaji wa dawa hizo amewatoa hofu wananchi  na kuwahakikishia  kuwa dawa za kutosha zenye viwango stahili zitaendelea kupatikana  katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini na kuwataka wananchi kutoa kushirikiana na mamlaka husika kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa dawa zenye ubora wenye mashaka au uvunjifu wa sheria inayosimamia ubora na usalama wa dawa.

VIA: MO BLOG
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment