WIKI
hii kwenye Funguka na Risasi tunaye mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva,
Joseph Haule, ‘Profesa Jay’ ambaye anafunguka juu ya bifu kati ya Judith
Wambura ‘Jide’ na Mkurugenzi wa Vipindi na Utafiti wa Clouds Media,
Ruge Mutahaba.
Profesa Jay naye ametajwa katika sakata hilo kutokana na kushirikishwa
katika wimbo wa Joto Hasira ambao wengi wameutafsiri kuwa na vijembe kwa
Ruge.
Funguka: Mambo vipi Profesa, nimekutafuta ili nipate msimamo wako kwenye bifu kati ya msanii mwenzako (Jide) na Ruge.
Profesa Jay: Kwanza nianze kusema kuwa mimi sina upande wowote ambao ninaweza kuusimamia, sipo kwa Ruge wala kwa Jide.
Funguka: Kumekuwa na minong’ono mitaani kuwa upo upande wa Jide kwani
mmekuwa mkifanya kazi pamoja vilevile ni marafiki kwa muda mrefu na
ndiyo maana amekushirikisha kwenye wimbo wake wa Joto Hasira.
Unalizungumziaje hili?
Profesa Jay: Ishu siyo mimi kuwa upande wa Jide au wa Ruge, kitu ambacho
ninaweza kukizungumzia ni kwamba Jide alinishirikisha kwenye wimbo huo
hata kabla ya hilo bifu lao sijalifahamu. Mimi niliimba kutokana na
maudhui ya wimbo ulivyokuwa ukitaka. Kwa hiyo bado nasisitiza kuwa
sifungamani na upande wowote katika jambo hili.
Funguka: Kama ni hivyo, unachukuliaje suala la Jide na Ruge kufikia hatua ya kuburuzana mahakamani?
Profesa Jay: Kuhusu hilo, sitakuwa msemaji sana ila kwa jinsi
ninavyofahamu, Jide ni msanii mkongwe. Kama unakumbuka nilishawahi
kufanya naye traki kadhaa kama Bongo Dar-es-salaam na Niamini. Kikubwa
ni kwamba Jide anajiheshimu sana na nadhani kila anachokifanya anakijua
vizuri.
Funguka: Unamuongeleaje Ruge na uongozi mzima wa Clouds kuhusu sakata hili?
Profesa Jay: Binafsi siwezi kuwaongelea Clouds au Ruge kwa jambo lolote,
kwa sababu ninaamini na wao ni watu wazima na wanafahamu nini
wanachokifanya.
Funguka: Hivi karibuni tumesikia wasanii kadhaa wamejitoa kwenye orodha
ya wasanii watakaomsapoti Jide kwenye shoo yake ya Mei 31, vipi wewe
utakamua kama kawaida?
Profesa Jay: Nikutoe wasiwasi, mimi binafsi nitakuwepo kwenye shoo ya
Jide na nitapiga mzigo wa kufa mtu kumsapoti kwa akili yangu yote, nguvu
zangu zote na moyo wangu wote.
Funguka: Poa, nashukuru kwa ushirikiano wako, kazi njema.
Profesa Jay: Haina kwere.
No comments:
Post a Comment