Mkuu
wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki akiongea na waandishi wa
habari (hawapo pichani) kufafanua oparesheni ya kuwaondoa wavamizi wa
ardhi katika eneo la Madale na zoezi la Sensa ya watu na makazi leo
jijini Dar es salaam.
UFAFANUZI OPARESHENI YA KUWAONDOA WAVAMIZI WA ARDHI ENEO LA MADALE NA ZOEZI LA SENSA JIJINI DAR ES SALAAM WATOLEWA.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
24/8/2012, Dar es salaam.
Serikali
imesema kuwa haitayavumilia makundi ya watu wanaovunja sheria za nchi
kwa kuendesha vitendo vya wizi, uvunjaji wa nyumba, uporaji na uuzaji
wa ardhi kinyume cha sheria katika maeneo yanayomilikiwa kihalali
jijini Dar es salaam.
Mkuu
wa mkoa wa Dar es salaam Bw. Saidi Meck Sadiki ametoa kauli hiyo leo
jijini Dar es salaam kufuatia vurugu zilizotokea katika eneo la Madale
nje kidogo ya jiji la Dar es salaam kutokana na uamuzi wa serikali
kuwaondoa kwa nguvu wananchi waliovamia maeneo hilo.
Amesema
kuwa serikali haikukurupuka kuchukua hatua hiyo na kuongeza kuwa hatua
zilizochukuliwa zimezingatia kanuni na taratibu za kisheria zikiwemo
baraka za kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa.
“
Kufanyika kwa zoezi hili si kwamba serikali ya Kinondoni imekurupuka,
hata kidogo haijafanya hivyo, zoezi hili limefuata kanuni na taratibu
zote za kisheria ikiwemo uamuzi wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa
wa Dar es salaam na amri ya Mahakama”
Amefafanua
kuwa matukio yaliyotokea hivi karibuni katika maeneo hayo kwa baadhi
ya makundi ya wananchi hasa vijana waliobeba silaha za jadi
kuwashambulia, kuwajeruhi na kuharibu mali za wananchi wanaoishi katika
eneo la Madale kihalali kwa lengo la kuwaondoa kwa nguvu na kuyatwaa
maeneo yao ni jambo lisilokubalika nchini.
Amesema
kuwa licha ya jambo hilo kuwa la muda mrefu na serikali kuchukua hatua
za kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo kihalali
wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa baadhi ya wananchi wamekuwa
hawakubaliani na jambo hilo na hatimaye kuanza kuyavamia maeneo ya wazi
ambayo mengine yanamilikiwa na taasisi na makampuni.
Ameongeza
kuwa zoezi hilo la kuwaondoa wananchi waliovamia maeneo hayo
lilizingatia taratibu zote ikiwemo hatua ya serikali kuwapa taarifa
wahusika wote waliovamia maeneo hayo kuondoka wenyewe jambo ambalo
hawakulifanya.
“Kabla
ya kutumia nguvu kuwaondoa wananchi hao serikali iliwapatia taarifa ya
kuwataka kuondoka wenyewe jambo ambalo walilikaidi na kuendelea
kukalia maeneo hayo kinyume cha sheria.
“
Bado naendelea kusisitiza kuwa serikali ilifuata taratibu zote, kwanza
tuliwashauri wamiliki halali kwenda mahakamani kisha mahakama ikatoa
amri ya wavamizi hao kuondolewa na zaidi ya hapo walipewa taarifa ya
kuondoka wao wenyewe jambo ambalo hawakulifanya na hii inaashria
kudharau amri ya mahakama” amesisitiza Bw. Sadiki.
Aidha
Bw. Saidi Meck Sadiki amesema kuwa imebainika kuwa baadhi ya wananchi
wanaoendesha vitendo hivyo vya kihalifu sio raia wa Tanzania na
kukongeza kuwa tayari vyombo vya dola vinavyohusika vinaendelea na
uchunguzi wa suala hilo na tayari vinawashikilia watu 68 kwa kuhusika
na vurugu hizo.
Pia
ameonyeshwa kusikitishwa na baadhi ya watendaji wachache wa serikali
na viongozi wa siasa wanaoshabikia na kuhamasisha suala hilo na
kuongeza kuwa serikali inaendelea na uchunguzi wa suala hilo na
ikibainika hathua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Katika
hatua nyingine mkuu wa mkoa wa Dar es salaam amevipongeza vyombo
mbalimbali vya habari vinavyoendelea kuwahamasisha wananchi kushiriki
katika zoezi la Sensa ya watu na makazi na kuongeza kuwa hivi sasa
wananchi wana uelewa mkubwa juu ya zoezi hilo na wako tayari kuhesabiwa.
“Navishukuru
sana vyombo vya habari kwa kazi nzuri za uhamasishaji wa watu
kushiriki katika Sensa ya watu na Makazi japo vipo vichache sana
vinavyoendesha mijadala ya kuipinga”
Amesema
maandalizi ya zoezi hilo kwa mkoa wa Dar es salaam yamekamilika licha
ya kuwepo kwa malalamiko na madai ya baadhi ya makarani wachache
kutolipwa fedha za mafunzo jambo ambalo amesema mamlaka husika
zinalifanyia kazi kwa kuhakikisha kuwa ukamilishaji wa uhakiki na
uthibitisho wa majina yao unakamilika leo.
“Kwa
upande wa jiji la Dar es salaam wengi wameshalipwa fedha zao na kwa
wale wachache ambao madai yao yanashughulikiwa nawahakikishia kuwa
watalipwa kwa kuwa fedha yao ipo” amesisitiza.
No comments:
Post a Comment