Tuesday, August 7, 2012

BALOZI SEIF ATOA WITO KWA WAISLAMU NCHINI.


 Mke wa Makamu Wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Asha Bilal, Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi wakiwa pamoja na wana kamati wa mashindano ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika chuo cha Kiislamu cha Al Haramain Mjini Dar es salaam.
Mwanafunzi Rashid Seif Hamad kutoka Chake chake Pemba  akiwa katika meza ya mashindano ya kuhifadhi Quran hapo chuo cha Kiislamu cha Al Haramain Mjini Dar es salaamu akionyesha umahiri wake. Rashid  ameibuka msindi wa pili katika kuhifadhi Juzuu 30.
Jopo zima la Majaji wanaoendesha mashindano ya Kuhifadhi Quran katika chuo cha Kiislam cha Al Haramain Mjini Dar es salaam wakiendelea na upembuzi wa kupata washindi katika mashindano hayo.
Mwakilishi wa Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Iran Nchini Tanzania Sheikh Murtaza  akimkabidhi Mgeni rasmi Balozi Seif zawadi ya Quran iliyohifadhiwa katika mfumo wa kisasa wa Digital hapo katika mashinda ya kuhifadhi Quran Al Haramain Mjini Dar es salaam. Kulia ni Mwenyekiti wa Wanawake wa Kiislamu Tanzania { Bakwata } Ukti Shamim Khan.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa nasaha zake mara baada ya kushuhudia mashindano ya kuhifadhi Quran yaliyoshirikisha Wanafunzi kutoka vyuo mbali mbali vya Bara na Zanzibar.Kulia ya Balozi ni Kaimu Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Ali Muhidini.
Mkamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi zawadi ya Baskeli Mwanafunzi Khalifa  Ali Faki baada ya kupata ushindi wa Pili  wa Juzuu 3 kwenye kilelecha mashindano ya kuhifadhi Quran.Kulia ni Mwenyekiti wa Waislamu wanawake Tanzania { Bakwata } Ukti Shamin Khan.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi mshindi wa kwanza wa mashindano ya kuhifadhi Quran Juzuu 30 Mwanafunzi Abdullhamid Masoud zawadi za Laptop na Printer katika mashindano hayo yaliyofanyika viwanja vya chuo cha Kiislamu cha Al Haramain Jijini Dar es salaam. Mwanafunzi Abdullhamid na wenzake mshindi wa pili na tatu pia wamefunguliwa akaunti kwa kianzio cha shilingi 1,000,000/- kila mmoja na Benki ya Amana Mjini Dar es salaam.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa katika picha ya pamoja na  Wajumbe wa kamati ya mashindano ya kuhifadhi Quran, Majaji pamoja na Uongozi wa Bakita ukiongozwa na Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Ali Muhidini Mgogoni.
Na Mwandishi Wetu
Waumini wa dini ya Kiislamu wamekumbushwa kuwa  tayari kuwarithisha  watoto wao mambo ambayo yanamridhisha  na kumfurahisha Mwenyezi Muungu likiwemo lile kubwa la kuhifadhi Quran Tukufu kwa lengo la kuwa na viongozi makini wa dini hiyo hapo baadaye.    
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi wakati akitoa nasaha zake kwenye  kilele cha mashindano ya kuhifadhi Quran yaliyofanyika katika viwanja vya Chuo cha Kiislamu cha Al-Haramain, Dar es Salaam.                
Balozi Seif alisema ni vyema kwa walimu wa vyuo vya Quran wakafikiria kufundisha kitabu hicho pamoja na tafsiri yake hata kwa kiwango cha Juzuu 15 ili kuwajengea vijana kupenda mambo yote mawili.                                                                             
Alisema kusoma na kuhifadhi Quran ni wajibu wa kila Muislamu ili ipatikane faida ambayo imekusanya mahitaji ya viumbe vyote hapa duniani.                                     
Alitahadharisha baadhi ya Waumini kujiepusha na tabia ya kutafsiri Quran kwa manufaa binafsi na kutoa wito kwa waumini hao kuendelea kushirikiana ili kuwa na nguvu katika mambo yao. 
“Ndani ya kitabu hiki kitakatifu kuna mahitaji yetu yote ya kilimwengu na kesho akhera. Tutapataje mahitaji yetu yote bila ya kuifahamu Quran Tukufu?” Alihoji Balozi Seif.                   
Aliipongeza kamati ya maandalizi ya mashindano hayo pamoja na wafadhili wote kwa juhudi za kufanikisha jambo hilo la kheri litakalowajengea hatma njema ya baadaye.
Balozi Seif alisema hakuna kujuta katika kutoa kwa vile uwekezaji huu malipo yake huendelea daima bila ya kikomo. Akizungumzia suala la mwezi mtukufu wa Ramadhani, Balozi Seif, aliwaasa waumini wenye tabia ya kusali kipindi cha mwezi mtukufu pekee kuacha tabia hiyo inayokwenda kinyume na maamrisho ya dini.
Alisema si vyema kwa waumini kuchagua mwezi wa kufanya ibada kwani muumini anawajibika kusimamisha sala kila siku katika kipindi chote cha siku 365 za mwaka mzima pamoja na kufanya mambo yote ya kheri.                                                
Mapema akisoma risala Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania iliyopo chini ya Bakwata, Ukti Shamim Khan alisema lengo la mashindano hayo ni kuwatia moyo vijana kuipenda Quran ambayo itawasaidia kuongoka kwa kuelekea kwenye ucha mungu.
 Ukti Khan alielezea masikitiko yake kuona walimu wanaowaandaa vijana hao kwa muda mrefu sasa wanasahauliwa. Alisema kazi yao ni nzito kinyume na kuangaliwa kama walimu wengine wa kawaida wanaotoa elimu ya dunia.                                                                                                              
 Alifahamisha kwamba elimu ya dini ni vyema ikaenda sambamba  na elimu ya dunia  katika hatua za  walimu hao kujengewa mazingira ya uwezeshaji.                         
Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo, Kaimu Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Ali Muhidini, alisema Quran lazima ifanywe kuwa dira katika maisha ya kila siku ya waumini wote.       
Sheikh Muhidini alisema ukosefu wa vijana wengi kutoelekezwa katika elimu ya dini kumesababisha utitiri wa watoto wa mitaani unaosababishwa na ukosefu wa malezi bora. 
“Mzazi kutompelekea mtoto wake kupata elimu ya Quran ni moja ya njia ya kuporomosha chini imani,” alisistiza.
Sheikh Muhidini pia amezionya baadhi ya kampuni za simu zinazoendesha utaratibu wa kutumia aya za kutoka kwenye Quran kuacha mara moja utaratibu huo ambao unadhalilisha kitabu kitakatifu cha Mwenyezi Mungu.                                                                                                                      
Zawadi mbalimbali zmetolewa kwa washindi wa mashindano hayo ikiwa ni pamoja na Laptop Printer, seti ya televisheni, misahafu, fedha taslimu ambazo washindi wamefunguliwa akaunti Benki ya Amana.
Mashindano hayo yamefadhiliwa na Benki ya Watu wa Zanzibar, Amana Benki pamoja na Rehema Foundatin inayofadhili wanafunzi katika vyuo mbali mbali ndani na nje ya nchi.
MWARICK JAPHET MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment