Tuesday, August 21, 2012

WARAKA WA RAIS WA TAFF KWA MAHARAMIA WA FILAMU


Simon Mwakifwamba
Simon Mwakifwamba Rais wa Shirikisho la Filamu Swahiliwood.
HAKUNA mtu asiyependa maendeleo ya mtu mwingine ambayo ni halali, lakini mtu anapobaini kuwa haki yake imeibiwa na kubaini mwizi ni ndugu yake ambaye yupo karibu naye upata maumivu makali yasiyosemekana, miaka inazidi kwenda filamu zinatakaa mitaani na kuifanya jamii iamini kuwa uigizaji ni kazi inayolipa kuliko kazi nyingine japo ukweli ipo hivyo lakini si kwa Tanzania, unapokuwa Tanzania kazi ya msanii haina ulinzi jambo linalotoa fursa kwa maharamia kujinufaisha.

Simon Mwakifwamba
Simon Mwakifwamba Rais wa Shirikisho la filamu akiongelea jambo fulani.
Hivyo basi kwa umoja wetu tunaungana na kuamua kwa moyo wa dhati kupigana na maharamia hawa wananyonya jasho letu pasipo huruma, kwani wanajulikana na tunaishi nao ni rafiki zetu lakini hawana huruma na sisi wanaamua kutunyonya hadi wahakikishe damu yote inamalizika kabisa na wao kuendelea kuneemeka hilo si sawa hakuna kitu cha rahisi lazima uvune kutokana na jasho lako, wasanii wamekuwa wanyonge kimaslahi pamoja na kutoa filamu zao kila kukicha hili si jambo la kulifumbia macho hata kidogo.
Tunaambiwa Maharamia wana mtandao lakini mtandao wao umefikia ukingoni kwani tayari tumeamka na kuamua kuingia katika mapambano na maharamia hawa ambao wamekuwa wakizorotesha juhudi za wananchi kubuni ajira na kujiajiri katika tasnia ya filamu, hivi karibuni mtuhumiwa aliyekamatwa na kazi za wasanii nakala kwa nakala huku akiwa na mashine za kurudufu kazi za wasanii alikuwa huru sana kwani hakuwa na hofu hata kidogo hata aliamua kufunga mitambo yake katika nyumba yake anayoishi bila kuwa na taadhari.
Jacob Stephen, Simon Mwakifwamba, Vincent Kigosi.
Rais wa TAFF Simon Mwakifwamba akiwa na JB na Ray wakiongelea suala la wizi kazi za filamu.
Hivyo basi kwa niaba ya shirikisho ningependa kuipongeza serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na bunge lake tukufu kwa ujumla kwa kubeba majukumu mazito na kufanikisha kuifikisha nchi hii mahali tulipofika ikiwa ni
pamoja na
1. Kupitisha kwa kauli moja kufanya marekebisho ya katiba ya nchi
2. Kusajili na kuwapa vitambulisho watanzania
3. Kufanikisha uwezeshaji wa sensa za watu na makazi
4. Na mengine mengi
Kama wasanii tunalitambua uwezo na ukakamavu mkuu wa serekali yetu tukufu ndio maana hatusiti kuwapa pongezi zetu za dhati na kuhimiza jamii kujitokeza na kuiunga serikali yao mkono kufanikisha malengo haya kwa haraka na
ufanisi mkubwa.
.
Jacob Steven
JB mwenyekiti wa Bongo Movie Unity ni moja kati ya wanaounda timu ya kupambana na Maharamia wa kazi za wasanii.

Tukirudi kwa upande mwingine sote tunafahamu mahali sisi wasanii tulipokuwa, mahali tulipo sasa na pengine tunapotarajia kufika. Kama mtoto mchanga tulianza kwa kuketi chini, tukaanza kutambaa, tumeanza kutembea ndiyo
tunatarajia kukimbia. Nyota yetu ndio inaanza angalao kung’aa na kuwa na ndoto na njozi nzuri kwa ajili ya urithi wa
wana wetu, lakini………………
Utamaduni wa mtanzania na utanzania wenyewe unaidhinishwa kupitia sanaa, elimu kwa jamii nzima unajumuishwa katika sanaa, maadili ya kitanzania unabebwa na kusambazwa kwa jamii kupitia sanaa, dini, uungu na utakatifu unaidhinishwa katika sanaa, wana siasa wote wanatengenezwa na kukuzwa kwa kiwango kikubwa sana na sanaa.
Wafanya kazi watiifu na wenye bidii kwa jamhuri hii wanajengwa na sanaa, wagonjwa wote wanaliwazwa na sanaa, waliofiwa wanaliwazwa na sanaa, wanandoa na harusi zote zinatimizwa na sanaa, habari na utangazaji vinabebwa na
sanaa, hivyo basi sanaa ndiyo inafanya kila kitu kiwe kama vile kilivyo, inastahili kuheshimiwa na si kudharauliwa
kama vile ilivyo sasa.
Nchi za ulaya zimejikita katika kukuza raslimali watu na kuenzi kile kitokanacho na raslimali watu hawa, mtu yeyote au kitu chochote ambacho kinaweza kuwazuia hawa raslimali watu kutimiza wajibu wao, basi inakuwa jukumu la kila mtu
kutatua tatizo hilo, huu ni mfano wa kuigwa.
Sanaa ina uwezo mkubwa sana katika kuengeza pato la nchi hii kwa zaidi ya asilimia 40%, kusaidia kuengeza ajira kwa vijana kwa zaidi ya asilimia 50% kuliko sekta nyingine yeyote, kuitambulisha nchi hii kimataifa(sasa hivi kupitia
MNET na television zingine zakimataifa)Kufanya Tanzania kuwa nchi yakitalii, kuchangia kujenga nchi hii kisaikolojia (wananchi watanzania na wageni wanapata faraja na kitulizo cha akili kupitia sanaa) huu ni mchango mkubwa sana katika taifa hili.
Mazuri haya yanatamanisha, na kila mtu anatamani na iwe hivyo, yote haya yanawezekana lakini hali kiukweli si hivyo,
wasanii wanalalamika, wazalishaji wanalalamika, wasambazaji wanalalamika, watumiaji wa kazi za sanaa walengwa wanalalamika, wanasiasa wanalalamika pia, serikali inalalamika kukosa ushuru lakini MTU MMOJA au WACHACHE wanafurahi, hawa si wasanii, wala wazalishaji au wasambazaji bali ni WEZI wa kazi za sanaa. Watu wengi wanapenda nyama sana lakini bucha za nyama ni chache kuliko library za kuuza kanda Bandia (Feki) zilizodurufiwa mtaani na hata mjini, hata upofu analiona na kulifahamu hili.
Tunabani CD na kuweka nyimbo kwenye flash, memory card haya ni maandishi tunayokutana nayo kila siku ukutani na kwenye vibao popote tuendapo Tanzania nzima hili si jambo geni, jamani huu si wizi kama wizi mwingine? Huyu msanii, mzalishaji au msambazaji atalipwa vipi? Na hili ndilo jembe lake, mbona mahindi zikiibiwa shambani mkulima analia na kulalamika vikali na hatua inachukuliwa, ngombe zikiibiwa watu wanjumuika kufuatilia pamoja na polisi wakibeba bunduki, hivi huyu msanii anaibiwa hadharani, mbele za ofisi za COSOTA wapo hapo nje, mbele za vituo vya polisi utakuta kanda feki inatembezwa hadharanibila uwoga, mbona hawa wasanii pia ni watoto wa watu kama vile watoto wengine?
Rigobert Massawe
Mtuhumiwa wa Wizi wa filamu za wasanii aliyekamatwa na filamu feki mamia kwa maalfu.
Ukiuliza mbona hivi, jibu la kwanza hatuna elimu, hatujui, hatuna ufahamu na filamu au muziki ikianza inaanza na ONYO hivi wanawezaje kuona kilicho ndani na wasione onyo, hivi hii elimu itoleweje? Mbona ilani za hamna njia hapa watu wanaona lakini inakuaje hawaoni ilani na onyo inayoanza kwenye filamu? Au muziki? Madereva wa basi wanaona vithibiti mwendo zilizoko kwa umbali barabaranilakini wanashindwa kuona ilani au onyo inayosema hairuhusiwi kuonyesha kwenye halaiki ya watu ambayo anaweka mwenyewe kuburudisha wasafiri wake, viongozi wa dini wanafundisha watu wasiibe na wao ndio wananunua kazi za wizi-feki mtaani, pengine kwa kutojua kuwa ni kazi bandia
Sisi wasanii tumebaki njia panda na tunaona na kuchukulia jambo hili kama dharau na ufanyaji mambo kimakusudi na
ukatili bila ya kujali maumivu makali anayopata mwenzio.
Hata hivyo ingawa tunaumizwa na kustahimili maumivu makali kutokana na maharamia hawa wa wizi wa kazi za sanaa tunapata faraja na moyo tukikumbuka agizo la Dr. Mohamedi Gharib Bilali, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania alilotoa mnamo mwezi October 2011 akiwa katika uzinduzi wa kanuni na sheria za Filamu na michezo ya Kuigiza mjini Musoma akiagizakukamatwa kwa maharamia wote wa kazi za filamu nchini kwa mbinu yoyote ile na wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Tamko hili linanguvu sana na linaonyesha uwajibikaji wa serekali ili kuokoa sekta hii ambayo sasa inayumbayumba inashiriki kilio cha samaki anayeliwa pande zote na kubakizwa mifupa tu, ila mtaji wa maskini ni nguvu zake kama
wasemavyo wahenga, TAFF, SHIRIKA LA KUTETEA HAKI ZA WASANII TANZANIA (SHIWATAN) likishirikiana Wadau/Wasanii wa Filamu na Muziki, Kampuni za Uzalishaji filamu, Kampuni za Usambazaji wa Filamu, Kampuni zinazo miliki bendi za Muziki na watu wote wenye uchungu na uzalendo kwa pamoja tumeamuakulivalia njuga na kulishughulikia tatizo hili ipasavyo bila kulalamikia mtu, chombo au taasisi yeyote.
Hili limedhihirika wazi mnamo jumanne tarehe 7 mnamo saa tatu asubuhi pale tulipopata taarifa za kuaminika kutoka kwa watanzania wazalendo kuhusu mtu Fulani anayedurufu kazi za wasanii mbalimbali za nyimbo na filamu, kwa kauli moja tulifahamisha polisi na kwa mpangilio madhubuti tukavamia duka lake na kufanikiwa kumkamata na kukamata
kazi nyingi sana na mitambo ya kisasa aliyokuwa anatumia kufanikisha uhalifu huo.
Kazi zilizokamatwa na polisi ziko katika mfumo wa DVD na VCD, pia kulikuwa na kava nyingi za wasanii mbalimbali makasha ya kuhifadhi DVD na VCD, Baadhi ya Filamu hizo ni Hatia 1 & 2 (Hisani Muya, almarufu kama TINO),The
Glory of Ramadhani 1& 2 (Vicenti Kigosi, almarufu kama RAY), Nakwenda kwa mwanangu 1& 2 (King Majuto na JB) Oprah 1& 2, the Twins 1 & 2 zinazomilikiwa na Game 1st quality zikiwa pamoja na Muziki mpya wa Jahazi (mpenzi Chokolate, MZEE YUSUPH).
Kazi za Injili za Kampuni ya MBC Hot Media, hizi ni baadhi tu ya kazi za wasanii zilizotajwa mtuhumiwa alikutwa na kila aina ya kazi za wasanii. Hii ni pamoja na gari lilosheheni kazi bandia (feki) alilokuwa anatumia kusambazia kazi
hizo kwa urahisi.
Mtuhumiwa alifanya uharamia huu kwa kutumia akili na ujuzi wa hali ya juu na kutumia mitambo ya hali ya juu sana kiasi kwamba huwezi kutambua iliyodurufiwa na kazi halali, pia aliweka stamp inayong’aa kuthibitisha uhalali wa kazi
hizi, hii inaonekana kuwa amefanya kazi hii kwa muda mrefu sana bila ya kugundulika na mtu yeyote kiasi kwamba alikuwa anauza hadharani bila uwoga.
Shirikisho na wadau wote wanapenda kutoa pongezi na shukrani za dhati kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Dr. Fenella Mukangara pamoja na Naibu waziri wa Wizarawa hiyo kwa kuwa bega kwa bega nasi katika zoezi hili la msako wa maharamia, IGP Said Mwema na Makamanda wa Mikoa pamoja na OCD wote kwa kutuunga mkono katika juhudi zetu za kupambana na Maharamia.
Jambo hili linaashiria kuwa maharamia hawa ni wengi na wamekita mizizi na kufanya kazi hii bila kugundulika kwa muda mrefu sana kiasi cha kuwafanya wao kuwa matajiri wenye vitu vya thamani huku wasanii maskini kama samaki
wanabaki wakilia huku wanaliwa pande zote mbili na kubaki mifupa.
Ndugu Wanahabari Kutokana na tukio hilo, Shirikisho la Filamu Tanzania na kamati yake kwa niaba ya Wasanii wote wa filamu na Muziki, Vyama Wanachama wa Shirikisho, Wasambazaji na kampuni zinazofanya kazi za Filamu na Muziki tunatoa tamko la Kulaani vikali Uharamia uliofanywa na kampuni ya Ndugu Rigobert Massawealmaarufu kwa jina la Msukuma wa hapa Dar es Salaam, ambaye amekuwa akikamatwa kila mara na kushindwa kupata adhabu stahili.
Bwana Rigobert Massawe ni mmoja kati ya Maharamia wakubwa wa kazi za filamu hapa nchini kwa kipindi kirefu, mwenye mbinu za kimataifa za uharamia, mwenye kujiamini kupita kiasi asiye na hofu na Sheria wala Serikali.Zoezi hili la kupambana na maharamia Papa kama Rigobert Massawe ikiwa na wale maharamia wadogo ambao wanajinufaisha kwa jasho la wasanii linaendelea bila kikomo, kwani tayari tumebaini maeneo maarufu kwa wizi huo ambayo ni Yombo, Tegeta, Banana, Buguruni na Mbezi mwisho tutawakamata na kuwashughulikia ipasavyo.
Aidha pia kupitia tamko hili tunaiomba Serikali ishughulikie mambo yafuatayo;
a. kumshugulikia mtuhumiwa huyu haraka ipasavyo ili iwe fundisho na kukomesha uharamia wa kazi za sanaa nchini
b. Kushughulikia haraka sheria mpya ya hakimiliki pamoja na sheria mpya ya TRA
c. Taasisi za Serikali zinazoshughulikia masuala ya sekta ya sanaa na Wasanii nchini kuwajibika ipasavyo.
d. Kuwaonya MACHINGA wote wanaotembeza DVD/VCD ambazo si halali waaache mara moja, pia Uonyeshaji wa Filamu kwa njia ya waya (Cable operators).
e. Vibanda umiza yaani wanaonyesha mitaani bila idhini ya wamiliki waache mara moja.
f. Kuwaonya watu wanaojishughulisha na uchomaji wa kazi za filamu, muziki kwa kutumia Kompyuta.
g. Tunawaonya wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kama Anga, majini na nchi kavu kama Mabasi yanayoenda Mikoani kuacha mara moja kuonyesha filamu hizo bila idhini ya wamiliki.
Niwahakikishie kwamba kuanzia leo na kuendelea yeyote ambaye atafanya hujuma katika kazi za Wasanii tutapambana
naye hata kama hujuma hiyo itafanywa kwa DVD/VCD/CD mbili za kazi yoyote ya Sanaa.
.
Mohamed Mtunis, Muhsein Awadh Msama
Mtunis akiongea na wanahabari hapo pichani kuhusu wizi wa filamu katika Hoteli ya De Mag iliyopo Mwananyamala.
Ndugu Waandishi wa habari tunatambua mpango wa serikali wa kuleta mabadiliko katika sekta ya filamu na muziki nchini lakini bila ya kufanyika jitihada za makusudi kudhibiti maharamia hawa urasimishaji unaotarajiwa kufanywa na Serikali hautakuwa na maana kwa sababu maharamia ni watu wenye mbinu katika kufanya wizi wao.
Lakini pia tunapenda kuwajulisha kwamba kutokana na kukithiri kwa matukio ya wizi wa kazi za sanaa nchini; Wasanii, Wadau wa filamu, Kampuni za Uzalishaji, Kampuni za Usambazaji wa Filamu, Shirikisho la Sanaa za Ufundi, Shirikiksho la Muziki nchiniwameomba kufanyike kwa matembezi ya kulaani wizi huo ambao umeshamiri zaidi ya miaka ishirini sasa ili kuonesha hisia za wizi huo, jamii pamoja na serikali itambue kuwa TUMECHOSHWA NA WIZI UNAOJULIKANA
Mwisho nawashukuru kwa ushirikiano wenu nanyi tunaomba kushiriki kikamilifu katika kusaidia Wasanii Tanzania.

PAMOJA TUIKUZE NA KUISIMAMIA TASNIA YA FILAMU NCHINI.
AHSANTENI.
SIMON J. MWAKIFWAMBA
RAIS SHIRIKISHO LA FILAMU TANZANIA.

VIA: http://filamucentral.co.tz
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment