Hivi majuzi niliskia kuwepo kwa tuzo za waandishi wa habari za mtandaoni maarufu kama waandishi wa magazeti tando (blogs). Katika Tuzo hizo ambazo ziliandaliwa kwa vigezo wanavyovijua Vodacom, wametajwa washindi fulani. Kama mdau wa kawaida katika magazeti tando, miongoni mwa waasisi wa Bloger wa kwanza kabisa wa Kitanzania naamini kwa sasa kama nchi hii itakuwa inaendeshwa kishkaji, kirafiki, kima kundi na ikaachwa bila kukemewa basi siku si nyingi tutapoteza ladha ya mashindano yanayopima viwango na ubora wa kazi hali itakayofanya nchi kubakia kuwa ya wababaishaji kila siku.

Eneo hili la magazeti tando niliwahi kulilalamikia kutokana na kukosekana ubunifu hasa inapotokea habari moja inajaa kila blog kama ambavyo ipo katika magazeti ya Tanzania. Kwa kuona hili hili nashangaa blog iliyo na kazi ya kubandika picha za magazeti ya kila siku ama habari za wasanii walio nje au kuchota mawazo ya watu katika FB na twitter, au kusubiri taarifa za Maafisa Habari ikaibuka mshindi kwa kuwa tu eti inaonesha kuwa na wasomaji wengi. Kwamba hamjui kuwa ukiseti weblog yako ihesabu wanaoitembelea itahesabu bila kujali ni nani anaingia mara ngapi?

Kwa mantiki hii kigezo cha idadi ya watu si muwli kuonesha kuwa huyu ni mahiri katika kutoa taarifa katika Blog yake.

Natoa rai, kuwa mliopata nafasi ya kuwa na nguvu katika makampuni msitumie nafasi hizo vibaya kwa kutaka kuidhinisha udhamini wa blog kwa rafiki zenu na kisha kupoteza ladha ya ubunifu katika blog. Najua mmefanya hivi sana katika maeneo kama ya sanaa za urembo na kwingineko lakini kumbukeni hili limezidi na haliwezi kuvumiliwa! Jamhuri hii ilikuwepo kabla yenu na hiki mnachojivunia kwa kuwa kimetengenezwa na urithi wa Baba zenu msitarajie kitabaki kuwa hivi kila siku. 

Tendeni haki japo kidogo jamii hii itawaheshimu.

Kwa masikitiko na hasira kidogo nawasilisha!
Bonny Makene Road to PhD.