Thursday, August 2, 2012

APONGEZWA KWA KUSAIDIA KUKAMATWA KWA GARI ILIYOSABABISHA AJALI YA KIFO


Na. Luppy Kungalo wa Jeshi la Polisi Dodoma,

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma limempongeza kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la Ally Augustino umri wa Miaka (20) baada ya kufanya kitendo cha kijasiri kwa kudandia gari lililosababisha ajali na kukimbia, kisha kufanya mawasiliano na askari Polisi mkoani humo na kufanikisha kukamatwa kwa gari hiyo.

Akizungumzia Tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamisha Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Bw. ZELOTHE STEPEN alisema lilitokea majira ya saa mbili usiku jana katika kijiji cha Chilonwa Wilayani Chamwino na kusababisha kifo kwa mtembea kwa miguu aliyejulikana kwa jina Daniel Chilomboli, mgogo mwenye umri wa miaka (30)

“ Gari lilipomgonga mtembea kwa miguu huyo lilipunguza kasi kidogo  na kusimama lakini kwa kuwa watu walikuwa wakipiga mayowe na kukusanyika kwa wingi Dereva aliwasha gari na kuanza kuondoka ndipo Kijana huyo bila kuchelewa akalidandia kwa nyuma na kuanza kufanya mawasiliano na Askari kwa kutumia simu” alielezea Bw. Zelothe Stephen

Alilitaja gari lilosababisha ajali hiyo ya kumgonga mtembea kwa miguu  kuwa ni lenye usajili wa namba T.775 ATD  MITSUBISHI CANTER ambalo ubavuni lilonyesha kumilikiwa na Bw. NJIUKA E.R.M WA SANDUKU LA Posta 1018 Dodoma.

Kamanda ZELOTHE STEPEN alipongeza kitendo Cha kijasiri kilichofanywa na kijana huyo kwa kutambua na kutekeleza kwa vitendo  Mkakati wa Polisi Jamii na Ulinzi Shirikishi ambao Jeshi la Polisi linahitaji ushirikiano huo sana toka kwa Wananchi .

“Natoa wito kwa wananchi wote kuiga mfano wa kijana huyu katika maeneo yenu na kuwa na uchungu dhidi ya  watu wasiotaka kufuata sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani kwa kuwafuatilia na kuwatolea taarifa katika vituo vya Polisi ili sheria ichukue nafasi dhidi yao” alitoa wito Kamanda Zelothe.

Bw. Zelothe alisema juhudi za Kulifuatilia gari hilo huku kijana Ally Augustino akiwa amedandia gari hilo lilihusisha pia mawasilianao na Mtendaji wa kata wa eneo hilo la Chilonwa Bw. Emanuel Matewa ambaye alichukua hatua kupiga simu kwa walinzi  wanaokusanya ushuru wa magari akatika eneo hilo la Chilonwa ambao nao walidhibiti eneo lao lakini gari hiyo ilipita njia nyingine.

Aidha Kamanda ZELOTHE STEPEN alisema mawasilianao yaliendelea kufanyika baina ya Kijana huyo na Askari wa Wilaya ya  Chamwino na Dodoma mjini na kufanikiwa kulikamata baada ya Dereva kuonyeshwa alama ya kusimama na askari, na yeye kusimama kisha kufungua mlango na kukimbia kusikojulikana.

Mkuu huyo wa Polisi Mkoa wa Dodoma alisema gari hilo lilikamatwa maeneo ya Chaduru  katika barabara iendayo eneo la Ipagara katika Wilaya ya Dodoma Mjini  na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka Dereva wa Gari hilo ili kuweza kumfikisha mahakamani kujibu shitaka linalomkabili.

Bw. ZELOTHE amesema tayari maelekezo yameshatolewa kwa Mkuu wa Usalama Barabarani katika Wilaya ya Chamwino kupitia katika vikundi vya Ulinzi Shirikishi katika eneo hilo kwenda kumpongeza kijana huyo na kuwahamasisha wengine waige tabia hiyo ya kishujaa.

Kamanda ZELOTHE STEPEN alitoa Rai kwamba kitendo kilichofanywa na kijana huyo, kiwe chachu kwa   wananchi katika maeneo yao na  kufungua  ukurasa mpya wa ushirikiano wa hali na mali, na utakaowezesha kuunganisha nguvu kati ya Jamii na Polisi na Wadau wengine dhidi ya kero za uhalifu  katika maeneo yao.
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment