Wednesday, September 7, 2016

Darasa la saba waanza mitihani leo



WATAHINIWA 795,761 wanatarajia kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) unaofanyika leo na kesho nchini kote.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk Charles Msonde alisema wanafunzi 372,883 ambao ni sawa na asilimia 46.86 ni wavulana na wasichana ni 422,878 ambao ni asilimia 53.14.


Mwaka 2015 watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 775,729 huku 763,602 ndio waliofanya mtihani huo na wanafunzi 518,034 walifaulu.


Dk Msonde alisema watahiniwa 765,097 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 30,664 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia. Masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa.


Alisema watahiniwa wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani ni 95 wakiwemo wavulana 57 na wasichana 38 wakati wale wenye uoni hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa ni 810 ambao kati yao wavulana ni 402 na wasichana ni 408.


“Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika kiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, fomu maalum za kujibia mtihani na nyaraka zote muhimu katika halmashauri na manispaa zote nchini,” alisema Dk Msonde.


Aidha, Dk Msonde alitoa mwito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri kuhakikisha taratibu za mitihani ya Taifa zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya vituo vya mitihani yanakuwa salama, tulivu na kuzuia mianya ya udanganyifu.


“Wasimamizi wanatakiwa kusimamia kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Nawaaasa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya Taifa,” alieleza.
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment