Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’.
Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’ akiwa na mkewe Wastara.
PAMOJA na
kwamba afya ya staa wa filamu Bongo, Sadick Juma Kilowoko ‘Sajuki’
inaendelea vizuri, imegundulika kuwa ana ugonjwa mwingine tofauti na ule
uliompeleka India kufanyiwa upasuaji,
Hivi karibuni, Sajuki alirejea kutoka nchini
India alipokwenda kwa ajili ya matibabu ambapo alionekana kuwa na
mabadiliko makubwa kiafya jambo lililowapa matumaini mashabiki wake.
HABARI MEZANI
Akizungumza na waandishi wetu, juzi, Jumapili nyumbani kwake, Tabata
jijini Dar es Salaam, mke wa Sajuki, Wastara Juma alisema mumewe
amegundulika kuwa na tatizo lingine walipokuwa nchini India kwa
matibabu.
Alisema, hawakutaka kuweka hali hiyo mapema kwa Watanzania
kwa kuhofia kusababisha simanzi, lakini sasa wanalazimika kufanya hivyo
ili kuwafanya wajue kinachoendelea kwa staa wao.
“Kwa kweli mume
wangu bado anaumwa na amegundulika kuwa na tatizo lingine ila
tunamshukuru Mungu anaendelea vizuri,” alisema Wastara kwa huzuni
nyingi.
NI UGONJWA GANI?
Kwa mujibu wa Wastara, walipokuwa
India (katika Hospitali ya Apollo), Sajuki alifanyiwa vipimo mbalimbali
ili kubaini matatizo yanayomsumbua ambapo aligundulika kuwa na tatizo
kwenye uti wa mgongo na ngozi ya mwili mzima.
“Ana tatizo kwenye
mfupa wa uti wa mgongo, lakini pia anasumbuliwa na tatizo jingine kwenye
ngozi. Baada ya madaktari kugundua magonjwa hayo walimuanzishia dawa ya
kutibu mgongo na mazoezi kwa ajili ya kumuweka sawa.
“Hizo dawa
alianza kuzitumia tulipokuja huku, ambapo pia anaendelea na mazoezi.
Tatizo lingine ni hilo la ngozi, ambalo pia anaendelea kutumia dawa,”
alisema.
KWA NINI MGONGO?
Akifafanua kuhusu ugonjwa
unaoshambulia sehemu ya mfupa wa uti wa mgongo, Wastara alisema
madaktari walisema, tatizo hilo linasababishwa na kukaa kwa muda mrefu.
“Jambo hilo tulikubaliana nalo, kwa sababu ni kweli Sajuki huwa anakaa
muda mrefu kwenye kompyuta kwa ajili ya kazi zake, lakini pia huwa
anaendesha gari kwa muda mrefu. Tunaamini ndiyo chanzo cha ugonjwa huo
kama madaktari walivyosema,” alisema na kuongeza:
“Lakini baada ya
kupata dawa na ushauri sasa anaendelea vizuri, kwa sababu pia anafuata
masharti aliyopewa vizuri. Huwa nahakikisha anapata muda mrefu wa
kupumzika, hakai muda mwingi na haendeshi sana gari.
“Wamemwambia
mambo mengi, hata kuinainama kila mara pia wamekataza. Kimsingi
mwenzangu anahitaji uangalizi wa karibu sana. Hata hivyo anaweza
kuendelea na filamu ila kwa kuzingatia na scene (onesho) yenyewe, ila
kwa sasa anapumzika kwanza ili afya yake itengemae.”
KLINIKI KILA WIKI
Akiendelea kuzungumzia afya ya mumewe, Wastara alisema huwa
wanalazimika kwenda Kliniki ya kila wiki katika hospitali moja jijini
Dar es Salaam kwa lengo la kuangaliwa maendeleo yake.
Aidha, alisema
kila wiki tatu huwa wanatuma vipimo nchini India katika Hospitali ya
Apollo aliyokuwa akitibiwa kwa lengo la kuchunguza maendeleo yake.
KUHUSU UGONJWA WA NGOZI
Wastara alisema, tatizo la ngozi alilonalo mumewe bado hajaanza kutumia
dozi yake kwa sababu hawajapata fedha ya kutuma India ili waweze
kutumiwa dawa zenyewe.
“Tupo kwenye mchakato wa kutafuta hizo fedha,
lakini hali bado ni ngumu na anatakiwa kuanza dozi mapema kama
madaktari walivyoshauri,” alisema na kuongeza:
“Mwezi Desemba (mwaka
huu) anatakiwa kurudi tena ili aangaliwe tena maendeleo yake kwa
ujumla. Yote hiyo ni gharama kubwa sana, lakini tunaamini Mungu
atatusimamia.”
GHARAMA ZAMTOA CHOZI WASTARA
Alisema kwa namna mahitaji yalivyo mengi na yanayohitaji fedha, wapo kwenye wakati mgumu kuweza kuyakabili.
“Kiukweli bado tunahitaji msaada wa Watanzania wenzetu. Tunashukuru kwa
wale waliojaliwa kutusaidia awali hadi kufanikisha safari yetu ya
matibabu India lakini watakaoguswa wanaweza kuendelea kutusaidia.
“Mpaka sasa Sajuki hajaanza dozi ya ugonjwa wa ngozi na zipo nyingine
anazotakiwa kuzitumia, lakini hazipatikani hapa...ni mpaka India.”
VIDUME VYAMTOKEA WASTARA
Akizungumzia suala la usumbufu wa kimapenzi, Wastara alisema ni jambo
la kawaida na ni kweli kuna baadhi ya wanaume wanatumia udhaifu wa
ugonjwa wa mumewe kumshawishi kimapenzi.
“Kutongozwa ni jambo la
kawaida kwa mwanamke, lakini mimi kama Wastara msimamo wangu ni
kumheshimu mume wangu. Siwezi kushawishika kwa namna yoyote, kwanza hata
hamu yenyewe sina.
“Ninachokiangalia kwa sasa ni afya ya mume
wangu. Najua nina wajibu mkubwa wa kuhakikisha namhudumia mume wangu kwa
mapenzi yote. Akili yangu haipo kwenye mapenzi kabisa, hali aliyonayo
mume wangu inaniumiza sana.
“Kamwe sitamsaliti Sajuki wangu. Wema
wake kwangu wakati nikiwa kwenye matatizo siwezi kuulipia kwa
kumdhalilisha kwa kutoka na mwanaume mwingine eti kwa sababu anaumwa.
Anayewaza kufanya hivyo, akajaribu kwingine, siyo kwangu.”
KALAMU YA MHARIRI
Kwa matatizo aliyonayo Sajuki ni wazi yeye na familia yake bado
wanahitaji msaada wa hali na mali ili kuweza kukidhi mahitaji ya
matibabu yanayomkabili kwa sasa.
Kama Mtanzania mwenzake, guswa na moyo wa utoaji na Mungu wa Mbinguni atakuongezea katika mifuko yako.
Ikiwa umeguswa, tafadhali tuma mchango wako kwenye akaunti namba
050000003047 yenye jina la Wastara Juma Issa iliyopo katika Benki ya
Biashara ya Akiba (ACB) au tumia Tigopesa kwenda namba 0713 666113 yenye
jina Wastara Juma.