Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus
Sabas akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kukamata madawa ya
kulevya aina ya Mirungi viroba 202 katika eneo la Engikareti lililopo
wilayani Longido Mkoa wa Arusha.
Baadhi
wa askari wa jeshi la polisi wakiharibu madawa ya kulevya aina ya
mirungi kwa kuikata kata na kisha kuimwagia mafuta. Mirungi hiyo
ilikamatwa katika eneo la Engikareti lililopo katika wilaya ya Longido
Mkoani Arusha.(Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi
la Polisi mkoani hapa limewakamata watu wanne wakiwa na madawa ya
kulevya aina ya mirungi. Watu hao walikuwa na jumla ya viroba 202 vya
madawa hayo ambayo yalikuwa kwenye gari aina ya Mitsubishi Canter lenye
namba za usajili T 306 BUN.
Akizungumza
na waaandishi wa habari nje ya jengo la Makao Makuu ya Jeshi hilo
Mkoani hapa, Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Kamishna Msaidizi wa Polisi
(ACP) Liberatus Sabas aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Joel Alfayo
Lukumay (37), Rahim Azizi Gilla (35), Ibrahimu Solomon Katambwei (40) na
Musa Lazaro Mollel (38) wote ni wakazi wa Mkoa wa Arusha.
Alisema
tukio hilo lilitokea leo saa 1:00 asubuhi katika eneo la Engikareti
lililopo wilayani Longido mkoani hapa. Aliongeza kwa kusema kwamba,
mafanikio hayo yametokana na taarifa toka kwa raia wema ambao
waliwasiliana na jeshi hilo, ambapo mara baada ya kupata taarifa hiyo
waliweka mtego katika eneo hilo na kufanikiwa kulikamata gari hilo
ambalo lilikuwa linatokea nchi jirani ya Kenya.
Kamanda Sabas aliwashukuru wananchi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano wao mkubwa
unaofanywa kwa jeshi hilo na kuwaomba waendelee kutoa taarifa za
uhalifu na wahalifu kwani kama wananchi wakiamua uhalifu unaweza
ukapungua kwa kiasi kikubwa.
Baadhi
ya waaandishi na askari waliokuwa kwenye eneo hilo walishuhudia viroba
hivyo vikiwa na majina ya watu pamoja na uzito wa kila mzigo huku
wengine wakidai kwamba inawezekana gari hilo huwa linabeba mizigo ya
watu mbalimbali ambao wanakuja kugawana mara baada ya kuingia Arusha
Mjini.
Kutokana
na tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoani hapa linaendelea kuwahoji
watuhumiwa hao na pindi upelelezi utakapokamilika watafikishwa
mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili. Aidha taarifa za ndani ya jeshi
hilo zinasema kwamba gari hilo lilishawahi kukamatwa tarehe 16 mwezi
Machi mwaka jana ambalo lilikutwa na madawa ya aina hiyo na kesi yake
ilikwishafikishwa mahakamani na bado shauri hilo bado linaendelea.
No comments:
Post a Comment