Tuesday, July 5, 2016

Mtoto wa Idi Amin akosoa sherehe za Entebbe


 
Bw Netanyahu amehimiza kuimarishwa kwa uhusiano baina ya Afrika na Isra


Mwanawe aliyekuwa kiongozi wa Uganda Idi Amin Dada amepinga sherehe za maadhimisho ya miaka 40 tangu kutekelezwa kwa operesheni ya makomando wa Israel uwanja wa ndege wa Entebbe.

Makomando hao walifika kuwaokoa mateka Wayahudi waliokuwa wanazuiliwa na wanamgambo wa Palestina waliokuwa wameteka ndege ya shirika la Air France.

Bw Hussein Lumumba Amin amesema ni makosa kwa serikali ya Uganda na nchi jirani za Afrika kushiriki sherehe hizo pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari, Bw Amin, anasema baada ya kutekelezwa kwa shambulio hilo 1976, Umoja wa Afrika ulilaani kitendo hicho.

Aidha, amesema si haki kwa babake, Idi Amin, kuoneshwa kama mhusika katika utekaji nyara wa ndege hiyo.

Anasema babake alikuwa anatekeleza wajibu wa mpatanishi na kwamba hata aliwafaa mateka waliokuwa wanazuiliwa.

Aidha, alikuwa anatetea haki za Wapalestina.
 
Mnara wa walinzi na waelekezi wa ndege uwanja wa Entebbe
“Kama Amin angekuwa anapendelea upande mmoja wakati huo, mateka hao huenda labda wangezuiliwa gereza kuu la Luzira au afisi iliyoogopwa sana ya makachero wa serikali ambapo hawangeweza kutoroka,” Bw Lumumba anasema.

Anasema Bw Amin aliwaokoa mateka hao kwa kuhakikisha ndege hiyo, baada ya kutekwa, iliweza kutua Libya na kuongezwa mafuta kabla ya kuendelea na safari hadi Uganda.
  • Netanyahu: Israeli inataka uhusiano na Afrika
Kabla ya hapo, anasema ndege hiyo ilikuwa inazunguka angani bahari ya Mediterranean na haikuwa na mafuta ya kutosha kufika Uganda.

Kiongozi huyo wa zamani, alimsihi kiongozi wa Libya wakati huo, Kanali Muamar Gaddafi, aruhusu ndege hiyo kuongezwa mafuta.

Wakati huo, Bw Lumumba anasema kwenye taarifa yake, serikali za nchi za Kiarabu zilikuwa zimekataa ndege hiyo itue nchi zao.

“Kuingilia kati kwake huenda kuliokoa mateka wote na wahudumu wa ndege kutoka kwa mkasa wa kuanguka baharini,” anasema Bw Lumumba.

Anaeleza kuwa uwanja wa ndege, Idi Amin, angewazuru mateka na alihakikisha walipewa chakula na malazi mema.
Mateka takriban 100 waliokolewa

“Habari zinazoenezwa kuhusu kisa hicho cha Entebbe zinafanya ionekane kana kwamba Amin mwenyewe alikuwa mtekaji nyara. Makusudi, wamekaa kimya kuhusu usaidizi wowote ambao huenda (Amin) alitoa kwa mateka hao wa Israeli wakati huo,” anasema Lumumba.

Nduguye Bw Netanyahu, Luteni Kanali Yonatan "Yoni" Netanyahu aliyeongoza makomando 29 wa Israeli ndiye pekee kutoka Israel aliyeuawa wakati wa operesheni hiyo.

Wanajeshi 20 wa Uganda waliuawa.
MWARICK JAPHET MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment