Siku
nne baada ya wamiliki wa maroli kupaki maroli yao kwa kigezo cha
kuhofia kuharibu barabara, Waziri Mkuu MIZENGO PINDA ameunda timu maalum
itakayoshirikisha wadau wa usafirishaji Mizigo na abiria, Wizara za
Ujenzi, Uchukuzi, Viwanda na Biashara Mambo ya ndani pamoja na Ofisi ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kutafuta suluhu ya mgogoro uliopo baina
ya wasafirishaji hao na Serikali.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Waziri Mkuu PINDA ametoa Mwezi mmoja kwa timu hiyo kuhakikisha inapata ufumbuzi wa mgogoro huo ili kulipunguzia Taifa hasara kiuchumi, inayoweza kusababishwa na hatua ya wasafirishaji hao kuamua kusitisha kuendelea kusafirisha Mizigo wakilalamikia utaratibu mpya wa Mizani uliotangazwa na Wizara ya ujenzi.
Aidha Waziri Mkuu PINDA amesema katika kipindi ambacho timu hiyo itakuwa ikiendelea kutafuta ufumbuzi wa suala hilo, ni vyema wasafirishaji hao wakaendelea na utaratibu wa awali wa vipimo vya mizigo na magari.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu PINDA amekiri kukithiri kwa vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi katika maeneo mbalimbali ya MIZANI nchini vinavyofanywa na baadhi ya watendaji wa TANROADS, Wasafirishaji wenyewe pamoja na watendaji wa Mizani hiyo.
No comments:
Post a Comment