Mgogoro ndani ya Chadema umezidi kupamba
moto baada ya Kamati Kuu kuwavua uongozi Zitto Kabwe na Dk Kitila
Mkumbo, huku Makamu Mwenyekiti Taifa, Said Arfi akiandika barua ya
kujiuzulu.
Zitto alivuliwa uongozi wa Naibu Katibu
Mkuu Taifa na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati
Dk Mkumbo amevuliwa ujumbe wa Kamati Kuu. Wawili hao wanatuhumiwa
kukisaliti chama.(HD)
Taarifa zilisema hoja ya kukisaliti chama
pia ilimkumba Arfi akidaiwa kumwezesha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kupita
ubunge bila kupingwa, katika uchaguzi mkuu uliopita na ndiyo sababu ya
kuamua kuachia ngazi nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Taifa.
Mbali ya kuwavua uongozi Zitto na Dk
Mkumbo, pia Kamati Kuu imewapa siku 14 wajieleze kwa nini wasifukuzwe
uanachama. Kwa uamuzi huo Zitto amebaki na wadhifa wa ubunge wake wa
Kigoma Kaskazini na wadhifa mwingine kwenye Kamati ya Bunge.
Zitto azungumza
Mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho,
Zitto aliliambia gazeti hili, "Sina cha kueleza, kikao kilikwenda
vizuri na taarifa rasmi ya chama kuhusu uamuzi wa kikao itatolewa
baadaye mchana (jana saa nane mchana), tusubiri Kamanda."
Arfi ajiuzulu
Makamu Mwenyekiti wa Taifa, Said Arfi
ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mpanda Mjini, jana aliwasilisha barua
ya kujiuzulu nafasi ya uongozi wa chama, akisema; "...kuchoshwa na
unafiki unaoendelea ndani ya chama. Napenda ifahamike pia kwangu
masilahi ya wapigakura, wakazi na wananchi wa Mpanda Mjini na Wilaya ya
Mpanda ni muhimu katika kuwatumikia, hivyo basi sipo tayari kuchaguliwa
marafiki.
Katika barua hiyo anasema amechochwa na
tuhuma ambazo zimekuwa zikielekezwa kwake kuwa alimsadia Waziri Mkuu
Mizengo Pinda kupita bila ya kupingwa katika uchaguzi wa ubunge katika
uchaguzi mkuu uliopita.
"Kwa kipindi kirefu zimekuwepo shutuma
dhidi yangu na kutiliwa shaka uhusiano wangu na Mhe Pinda Waziri Mkuu.
Pamoja na kulijadili katika vikao kadhaa Mpanda na Dar es Salaam bado
yapo mashaka kwa nini alipita bila kupingwa. Huo ulikuwa uamuzi wa
Wanampanda kwenu imekuwa ni tatizo, lakini hamsemi kwa nini. Majimbo
mengine 16 nchini yalipita bila kupingwa mlikuwa wapi na nani alaumiwe?
Huu ni unafiki wa kupindukia.
Vilevile, katika barua hiyo, Arfi anasema
amechukizwa na kauli ya mwasisi wa chama hicho, aliyemtaja kwa jina
moja la Mtei kuwachagulia marafiki.
"Aidha mmechukizwa sana kwa nini nilihoji
kauli ya Mwasisi wa chama, Mhe Mtei kutuchagulia viongozi. Naomba
ifahamike wazi kwamba huu ni mtazamo wangu na utabakia hivyo siku zote
kwa chama cha demokrasia kutoruhusu uongozi wa kiimla kwa kukidhi
matakwa ya waasisi ambao huvigeuza vyama kuwa mali binafsi.Kwa kusema
ukweli na kusimamia ukweli daima itabakia kuwa lengo langu katika maisha
yangu siku zote hata kama itanigharimu maisha yangu."
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk
Willbroad Slaa alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu barua ya Arfi ya
kujiuzulu uongozi, alisema; "Mimi nimekwishaondoka ofisini."
Taarifa ya chama
Akitangaza uamuzi wa Kamati Kuu jana
Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema, Zitto, Dk Mkumbo na
Mwenyekiti wa Chadema mkoani Arusha, Samson Mwigamba walikuwa na mtandao
wa kukiua chama hicho, huku wakitengeneza tuhuma za kuwachafua
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Katibu wake, Dk Willbroad
Slaa.
Alisema kuwa kamati kuu ilibaini kuwapo
kwa mkakati mkubwa wa watu hao kutimiza malengo hayo ambao umeandikwa
katika waraka unaoitwa 'Mkakati wa Mabadiliko 2013', ambao umeandaliwa
na kikundi kinachojiita 'Mtandao wa Ushindi'.
"Kikundi hicho vinara wake wapo wanne,
Zitto anajulikana kama Mhusika Mkuu (MM), Mkumbo (M1), Mwigamba (M3) na
mtu mwingine wa nne hatujamtambua kwa sasa yeye anatumia jina la M2"
alisema Lissu.
Alisema wakati wa kuhojiwa na Kamati Kuu
Dk Mkumbo alikiri kuwa mhusika mkuu wa mtandao huo ni Zitto, lakini
Zitto alikana kuutambua waraka huo licha ya kueleza unamhusu kwa kuwa
umetaja jina lake, kauli ambayo alidai Kamati Kuu haikutaka kuiamini.
Huku akieleza jinsi watu hao walivyokuwa
wakiwasiliana na kupanga mikakati ya kuimaliza Chadema kwa siri chini ya
ufadhili wa fedha kutoka kwa Zitto, Lissu alisema Naibu Katibu Mkuu
huyo wa zamani alikuwa akitumiwa na Chama Tawala (CCM) kuimaliza
Chadema.
"Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango
haramu na ambao unaichanachana katiba ya chama chetu. Ni mkakati wa vita
dhidi ya chama chetu na utaratibu wetu wa kikatiba. Hatuwezi kunyamazia
mkakati huu wa kutumaliza, uvumilivu umefika kikomo," alisema.
Uamuzi
Alisema kutokana na hali hiyo kamati kuu
iliamuru wahusika wote wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi wa chama,
kukubaliana kuunda timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa sekretarieti ya
makao makuu ya chama hicho ili kumtambua mtu wa nne (M2).
"Kamati ya Bunge imetakiwa kuchukua hatua
za haraka kuhakikisha Zitto anavuliwa nafasi zote za Naibu Kiongozi wa
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia wote wanatakiwa kujieleza ndani ya
siku 14 kwa nini wasivuliwe uanachama na watapewa fursa ya kujitetea,"
alisema.Alisema Kamati Kuu itakutana kwa dharura kwa ajili ya kufanya
uamuzi juu ya hatima ya watuhumiwa hao.
Kauli ya Mbowe
Awali Mbowe alipinga madai kuwa Zitto
ameondolewa kwa kuwa alikuwa akitaka kugombea nafasi ya uenyekiti wa
chama hicho, akasisitiza kuwa uamuzi huo umefanyika kwa kuwa Chadema ni
chama cha watu, siyo mali ya mtu binafsi.
Mvutano Zitto, Lema
Kwa zaidi ya wiki mbili Zitto amekuwa akilumbana na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho.
Vita hiyo ilianzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki iliyopita aliposema kuwa Zitto anafanya unafiki kukataa posho.
Alimtuhumu mbunge huyo wa Kigoma
Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho
nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya kijamii nchini.
Lema aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao
wa Jamii Forum huku akisema suala hilo halihitaji vikao vya chama
kulijadili isipokuwa vyombo vya habari na hususan, mitandao ya kijamii
kwani hata Zitto hutumia mitandao hiyo.
Zitto alijibu kuwa tangu siku nyingi
alikwishapiga marufuku kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati
hiyo.
Alisema tangu alipokuwa Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alipiga marufuku
posho na pia aliwahi kuwashtaki kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia
Rushwa (Takukuru) wabunge wanaochukua posho kutoka taasisi za Serikali.
Zitto pia alipata msukosuko mwingine
baada ya kusambazwa ripoti inayoitwa 'Taarifa ya Siri ya Chadema'
iliyomtuhumu kuwa alikuwa anashirikiana na CCM na viongozi wa Idara ya
Usalama wa Taifa kuihujumu Chadema.
Pia, Zitto aliingia katika malumbano na
chama chake baada ya kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake
hazikaguliwi na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), huku
akitaka ruzuku kwenye vyama hivyo isimamishwe.Chadema ilipinga vikali
madai hayo na kueleza kuwa imekuwa inatumia taasisi binafsi kufanya kazi
hiyo. Vyama vinavyopata ruzuku ya Serikali ni vile vyenye wabunge
Chadema, CCM, UDP, TLP, CUF na NCCR-Mageuzi.
Mvutano kikaoni
Wakati wajumbe wa kikao hicho wakivutana,
Zitto alikuwa njiani akirejea kutoka Sudan Kusini, ambapo alienda na
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho
zinaeleza kuwa, baada ya kuibuka sintofahamu hiyo, Mbowe aliwapoza
wajumbe wa kikao hicho, akiwaeleza kuwa haitakuwa busara kumjadili mtu
ambaye hayupo.
"Mbowe alipendekeza kuwa ajenda hiyo
iwekwe kando na itajadiliwa baadaye kutokana na Zitto kutokuwepo katika
kikao hicho," zilieleza habari hizo.
Baadaye Zitto alituma ujumbe ambao
ulitangazwa kwa wajumbe wote, kwamba alikuwa njiani kurejea Tanzania,
kwamba akifika moja kwa moja atakwenda katika kikao hicho.
Zitto awasili, mzozo waibuka
Kama vile alikuwa akisubiriwa yeye, mara
baada ya kufika katika ukumbi huo saa 2:23 usiku huku akisindikizwa na
walinzi wanne, mvutano mkali uliibuka katika ukumbi huo na mara kadhaa
walinzi wa chama hicho, Red Brigade walionekana kukaa tayari mlangoni
kuzuia vurugu kama ingetokea.
Gazeti hili lilikuwa nje ya ukumbi huo na
mara kadhaa lilisikia sauti za malumbano za baadhi ya viongozi wa chama
hicho, akiwamo Zitto, Mbowe na Lema.
Wakati wakitoa maelezo kwa nyakati
tofauti Lema na Zitto walishutumiana huku kila mmoja akimtaja mwenzake
kuwa anatumia vibaya nafasi yake na mitandao ya kijamii.
"Tatizo lake ni kutumia mitandao ya
kijamii kueleza mambo ya chama wakati akijua siyo utaratibu, ugomvi
wangu naye kwa kiasi kikubwa uko hapo," alisikika akisema Lema.
Kuna wakati yaliibuka malumbano makali
huku sauti za juu zikisikika kutoka ndani ya ukumbi huo, kati ya Zitto,
Lema na Mbowe.Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho zinaeleza kuwa Dk
Mkumbo alikumbwa na rungu hilo baada ya kubainika kuwa alikuwa ameanda
taarifa za siri ambazo zilikutwa katika kompyuta mpakato (laptop) ya
Mwigamba ambayo alinyang'anywa baada ya kudaiwa alikuwa anasambaza
taarifa za kuhujumu chama hicho.
Kikao hicho kilimalizika saa 10:00
alfajiri huku maamuzi hayo yakifanywa siri na Mbowe alipoulizwa kuhusu
kuwepo kwa taarifa za Zitto na Dk Mkumbo kuvuliwa uongozi," alisema ,
"Taarifa zitatolewa baadaye mchana."
Wasomi wazungumza
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa
Gaudence Mpangala alisema Chadema ni chama kikubwa kinachoweza kushinda
uchaguzi mkuu ujao hivyo kinapaswa kuwa na viongozi walioshikamana na
kuwa na nia moja.
Aliongeza kuwa endapo wapo viongozi
wanaoonekana kwenda kinyume na viongozi wenzao na kwenda kinyume na
misimamo ya Chama, kinayo haki ya kufanya maamuzi ya namna yoyote yenye
lengo la kukinusuru.
"Chadema ni chama kikubwa kinachoweza
kushika dola...kinahitaji mshikamano mkubwa kwa viongozi wake na
kuhakikisha hawatokei wasaliti....kama ni kweli waliosimamishwa ni
wasaliti ni halali kabisa" anasema Profesa Mpangala.
Naye aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
cha SAUT, Dk Charles Kitima alisema wakati umefika kwa vyama vya siasa
kutambua kuwa uwepo wa demokrasia ndani ya vyama vingi vya siasa nchini
ni kusahihishana na kujisahihisha.
Dk Kitima alisema kuwa na mitazamo
tofauti siyo usaliti ni demokrasia na kusema endapo mtu au kiongozi
anafanya kitendo cha kuvunja katiba ya nchi huyo moja kwa moja anakuwa
mkosaji.
Mbunge wa Jimbo la Wawi (CUF), Hamad
Rashid anasema matukio ya kufukuzana na kutuhumiana baina ya viongozi
yanayofanywa na watendaji mkuu wa vyama vya upinzani yatasababisha
upinzani uzidi kudidimia na kudumaa.
Alisema vyama vya siasa vimekuwa na
usultani wa kuonekana kuwa vinapaswa kuongozwa na baadhi ya watu, na
wengine wenye uwezo na mawazo mapya na yasiyopendwa na wakubwa
anatafutiwa mbinu ya kuondoka.
Rashid alisema hali hiyo inasababishwa na
kukosekana kwa mfumo mzuri wa uongozi ndani ya vyama vya siasa, ambapo
anasema vyama haviongozwi kama taasisi na badala yake vinaongozwa kama
mali za watu.
"Hili linalotokea Chadema sasa ni matokeo
ya mfumo mbovu wa uongozi ndani ya vyama vya siasa nchini....vingi
haviongozwi kama taasisi." alisema.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment