Tukio hilo lilitokea juzi saa 8:30 mchana na baadaye mvulana huyo aliyetambuliwa na Polisi kwa jina la Abdul Alpha (22) kujisalimisha katika kituo cha Polisi cha Stendi Kuu ya Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo, akidai alikuwa akitaka kutoroka lakini aliona amefanya dhambi kubwa.
Akizungumza na mwandishi jana, mama mkubwa wa marehemu, Mwajuma Khamis alisema Sharifa alimaliza kidato cha nne katika sekondari ya Luguruni na alikuwa akisubiri matokeo.
Alisema juzi waliporejea kutoka kazini hawakumkuta nyumbani, waliulizia kwa ndugu kutokana na kwamba hakuwa na tabia ya kutoka nyumbani, lakini hawakufanikiwa kumpata hadi jioni ndipo polisi walipowataarifu kupatikana kwa mwili wake.
Alisema mwili wa marehemu ulikutwa chumbani kwa kijana huyo karibu na nyumbani kwao ukiwa na majeraha mwilini, lakini hawakujua kama mtoto wao ana mwanaume, wanatarajia kumzika kesho saa saba mchana.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura alisema polisi walipata taarifa za tukio hilo katika kituo cha Ubungo na kwenda katika chumba cha kijana huyo kilichokuwa kimefungwa kwa ndani na kukuta mwili wa msichana huyo ukiwa umejeruhiwa.
Alisema baada ya kumhoji mtuhumiwa, alisema alifanya hivyo kutokana na wivu wa kimapenzi, kwani alikuwa na uhusiano na msichana huyo lakini wazazi wa msichana hawakutaka amwoe, hivyo kumtaarifu kuwa amepata mchumba mwingine.
Alipoulizwa kwa nini hakutoa taarifa katika kituo cha Polisi Kimara alikofanyia mauaji, alisema aliogopa watu wa maeneo yale wangempiga na kumwua, kwa kitendo hicho.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Tumbi, Kibaha, huku kijana huyo akishikiliwa na Polisi.
No comments:
Post a Comment