Dar es Salaam. Aliyekuwa
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Dk Kitila Mkumbo amezungumzia mambo
sita yaliyojitokeza baina yake na wajumbe wenzake kabla ya kutimuliwa
katika wadhifa huo.
Aidha, alisema alishiriki kuuandaa na kuuhariri ‘Waraka wa Mkakati wa
Mabadiliko 2013’ uliokuwa mahususi kumwandaa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu
wa chama hicho, Zitto Kabwe kuwa mwenyekiti.
Dk Mkumbo alivuliwa wadhifa huo akituhumiwa kufanya vitendo kinyume cha katiba na taratibu za chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mhadhiri huyo wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema: “Waraka ulilenga kujenga hoja ya
kufanya mabadiliko ya uongozi na kuainisha mikakati ya ushindi kwa
mgombea mlengwa katika Uchaguzi Mkuu wa Chadema ambao kwa ratiba ya
awali ulikuwa ufanyike Desemba mwaka huu.”
Alisema katika kikao cha Kamati Kuu kilichowavua wadhifa huo, wajumbe
walisema waraka huo ulikuwa na upungufu na ulikiuka misingi na kanuni
zilizoainishwa katika Katiba ya Chadema.
“Kwa kuwa dhamira yangu imekuwa ni kusukuma mabadiliko ambayo Watanzania
wanayatizama nje ya mfumo wa sasa wa utawala, nilikiri makosa na
niliomba msamaha na kuomba kujiuzulu nafasi zote za uongozi ombi ambalo
lilipingwa na wajumbe. Mwanasheria wetu akawashauri kuwa tukijiuzulu
tutaondoka na heshima zetu, akataka tufukuzwe ili tuondoke na aibu,”
alisema Dk Mkumbo. Alisema kunapokuwa na uchaguzi ndani au nje ya chama,
watu lazima wafanye mikakati akisema hata leo Chadema kunafanyika
mikakati ya kuiondoa CCM madarakani mwaka 2015 na kwamba kitendo hicho
siyo dhambi.
Alisema katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa ndani wa
Chadema, kuna haki ya kujiandaa… “Sisi tunaamini mabadiliko, mimi na
Mwigamba tulianza kutengeneza mkakati, kwanza tuainishe sababu za kutaka
mabadiliko, pili tutafute nani anayefaa kuwa mgombea wetu.”
“Tuliazimia kwamba tukimpata tuchambue nguvu na udhaifu wake na pia
kuchambua udhaifu wa mgombea tunayedhani atatoka upande wa pili.
Tulifanya hivyo kwa siri na ilikuwa siri kati yangu mimi na Mwigamba kwa
sababu mikakati ya uchaguzi ni siri.”
Alisema kuwa baada ya kukamilisha mchakato huo wangemfuata Zitto na
kumwomba kuwa mgombea: “Ndiyo maana tulieleza katika waraka kwamba
hatuna uhakika kama Zitto atakubali kugombea, tulitaka kufanya haraka
kukutana naye, ila uchaguzi ulipohairishwa nasi tukatulia.”
Alisema kikao cha Kamati Kuu kilipokutana Zitto alikuwa hajui lolote
kuhusu waraka huo, pia yeye (Dk Kitila), alikuwa hajui kama waraka huo
ulikuwa umevuja kwa wanachama wa Chadema, wakiwamo wajumbe wa Kamati
Kuu.
“Siamini kama kugombea nafasi yoyote ndani ya chama ni uhaini. Msingi
namba moja wa Chadema ni demokrasia ambayo inatakiwa kuruhusu ushindani
katika nafasi za uongozi na hasa wa juu. Wanasema uhaini kwa sababu ya
wasiwasi wa siasa za ushindani katika chama chetu, hakuna uhaini wala
hujuma,” alisema.
Alisema siasa za ushindani nchini hazijaanza leo na kutolea mfano jinsi
uchaguzi wa Chama cha Tanu alivyokuwa na ushindani kati ya Mwalimu
Julius Nyerere na Ally Sykes.
“Rais Barack Obama wa Marekani alianza mikakati mapema, waliomfikisha
pale alipo ni watu wanne waliotengeneza mkakati wa kupata mgombea na
kufanya ashinde bila Obama kujua,” alisema.
Alisema yeye na Mwigamba walitumia njia hiyo na kwamba baadaye
wangemfuata Zitto, wangembembeleza na wanaamini kuwa angekubali, “Siasa
za ushindani ndani ya vyama ndiyo huzaa ushindani wa kweli katika jamii
na kujenga demokrasia ya kweli katika jamii.”
Alisema waraka huo ulioandaliwa na watu wawili unaoeleza udhaifu na
nguvu ya Chadema ulikuwa siri, lakini anashangazwa kuona viongozi wa
chama hicho kuusambaza, huku akiwataka wanachama wa Chadema kuusoma
waraka huo na kueleza uhaini wao ni nini.
Alisema waraka huo haukulenga kukibomoa Chadema, bali kujenga taasisi na
kufafanua kuwa aliomba kujiuzulu nafasi yake si kwa sababu ya kuogopa
aibu ya kufukuzwa isipokuwa kutambua jinsi wenzake walivyokosa imani
naye.
Aliwataka wanachama wa Chadema kupigania kwa dhati misingi mama ya chama ikiwamo demokrasia ya ndani.
“Tutawashawishi Watanzania kwamba chama hiki ni cha demokrasia kwa sisi
wenyewe kuonyesha ushindani ndani ya chama. Hakuna namna ya kuweza
kudhihirisha hilo zaidi ya kuruhusu uchaguzi huru na watu washindane kwa
hoja,” alisema Dk Kitila.
Alisema wanachama wa Chadema wanatakiwa kulaani tabia iliyoibuka ndani
ya chama hicho kuwaita watu wenye mtazamo tofauti na viongozi kuwa ni
wasaliti. “Kukataa siasa za ushindani ndani ya chama ni kuhujumu
demokrasia na ndiyo usaliti, kukataa demokrasia na kukosolewa huo ndiyo
usaliti wenyewe.”
Alisema lugha za kuitana wasaliti au wahaini zilitumika katika mataifa
ya kikomunisti kunyamazisha upinzani na kuzaa udikteta kwenye mataifa
hayo, kwamba utamaduni huo ukilelewa Chadema utajenga udikteta.
No comments:
Post a Comment