Zaidi
ya wakazi elfu 25 wa mji mdogo wa Magu mkoani Mwanza wanalazimika
kutumia maji yaliyotuama kwenye madimbwi kufuatia uhaba mkubwa wa maji
unaoukabili mji huo kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu sasa.
Baadhi
ya wakazi wa mji huo wameeleza kuwa tatizo hilo limesababisha watumie
muda wao mwingi kuyatafuta maji ambayo wakati mwingine sio safi wala
salama kwa afya zao badala ya kufanya kazi za kuwaingizia kipato na
hivyo kuwaweka kwenye hatari ya kukumbwa na magonjwa ya milipuko.
Adha
ya ukosefu wa maji safi na salama katika mji wa Magu mkoani mwanza
inawalazimu wakazi wa mji huo kutembea umbali wa zaidi ya kilometa tano
ili angalau waweze kuambulia ndoo moja ya maji kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani kutoka katika vijiji jirani.
Wapo
wananchi wa magu wanaodiriki kujitosa katika madimbwi ambayo yana kila
ishara ya kukosa hadhi ya kutumiwa na binadamu kutokana na maji yake
kutuama.
Suala
la upatikanaji usioridhisha wa maji katika mji wa Magu pia limeibua
mjadala katika kikao cha baraza la madiwani la halmashauri ya wilaya
hiyo.
Hofu ya kuibuka kwa magonjwa ya milipuko sasa ni tele miongoni mwa baadhi ya madiwani wa magu.
mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya magu NAOMI NKO amekiri kuwepo kwa tatizo hilo.
Amicus Butunga, TBC Mwanza.
No comments:
Post a Comment