HATIMAYE PINDA KUWA WA KWANZA KUBURUZWA MAHAKAMANI ...Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimemfungulia mashtaka Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda kutokana na kauli yake aliyoitoa bungeni hivi
karibuni kwamba wanaokaidi maagizo ya dola wapigwe.
Hatua
hiyo ya LHRC imepingwa vikali na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP),
Dk Elieza Feleshi akisema hakuna uhalali wa mashtaka yoyote dhidi ya
kiongozi huyo sababu kauli ya Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua.
Mkurugenzi
wa LHRC, Dk Hellen Kijo Bisimba alifungua mashtaka hayo katika Mahakama
Kuu jana akisema kuwa wanamshtaki Waziri Mkuu kwa maelezo kuwa amekiuka
kifungu cha Katiba Ibara 13 (1). Pinda ametajwa kuwa ni mdaiwa wa
kwanza katika kesi hiyo namba 24.
Mkurugenzi
wa Maboresho na Utetezi wa LHRC, Harold Sungusia alisema jana kwamba,
mwingine aliyeunganishwa katika kesi hiyo ya kikatiba iliyofunguliwa na
LHRC na Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) ni Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema.
Alisema
katika kesi hiyo, kuna jopo la mawakili wasiopungua 20 na kwamba
wamepata saini za wananchi 2,029 wanaopinga kauli hiyo ya Pinda na
kuunga mkono kufunguliwa kwa kesi hiyo.
Mjumbe
wa Bodi ya LHRC, Wakili Dk Ringo Tenga alisema katika kesi hiyo
wameangalia zaidi sheria na hasa haki za msingi za binadamu na kwamba
kauli hiyo ya Waziri Mkuu Pinda inahatarisha haki hizo.
Kauli yenyewe
Wakati
wa Kipindi cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu bungeni, Juni
19, mwaka huu, Waziri Mkuu akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilwa
Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu aliyeuliza: “Serikali ipo tayari kiasi
gani kubainisha na kuchukua hatua stahiki, badala ya kusakama makundi
fulani, tujue chanzo halisi cha vurugu hizi na matatizo haya na jinsi
gani vyombo vya dola vinavyoshughulikia kwa sababu yapo malalamiko
katika baadhi ya maeneo kama Mtwara kwamba wananchi wanapigwa na vyombo
vya dola?”
Waziri
Mkuu alijibu: “Ni lilelile nililosema... mwishowe unaona anasema vyombo
vya dola vinapiga watu. Ukifanya fujo, umeambiwa usifanye hiki, ukaamua
kukaidi, utapigwa tu... hamna namna nyingine, maana wote tukubaliane
kwamba nchi hii tunaiendesha kwa misingi ya kisheria.
“Sasa
kama wewe umekaidi, hutaki unaona kwamba ni imara zaidi... wewe ndiyo
jeuri zaidi watakupiga tu.... Mimi nasema muwapige tu, kwa sababu hakuna
namna nyingine... maana tumechoka.” Kesi hiyo itakayosikilizwa na
majaji watatu, haina uhusiano na kesi nyingine ambazo wajibu maombi
hupewa siku 90 kujibu hoja zilizowasilishwa. Kesi hiyo imefunguliwa kwa
mujibu wa Katiba Sura ya Tatu.
Akizungumza
juzi kwenye Viwanja vya Bunge mjini Dodoma baada ya kufungwa kwa Warsha
ya Wapelelezi na Waendesha Mashtaka wa Serikali ngazi ya mikoa, Dk
Feleshi alisema hakuna uhalali wa mashtaka hayo kwa sababu kauli ya
Pinda kuwa pigeni haikuwa piga ua.
“Hii
haikuwa kuchochea apige watu, alichosema ni kupiga wale wasiotaka
kutekeleza amri halali na zaidi alisema piga lakini si kupiga na kuua,”
alisema.
Mkutano
huo uliendeshwa chini ya ulinzi mkali huku kukiwa na udhibiti wa kuvuja
siri kwa kiwango cha juu. Pamoja na mambo mengine, ulikuwa ukijadili
mbinu za kisasa katika kuendesha kesi pamoja na kujiuliza sababu za
Serikali kushindwa katika kesi nyingi.
“Kwa
sababu lile neno kupiga ni lazima lipewe maana pana huwezi kumpiga tu
mtu hivihivi ambaye hakuvunja sheria lakini nilivyoelewa, ilikuwa ni
hivyo, ni sawa na mtu ambaye anamshambulia askari,” alisema Dk Feleshi.
Alisema
kuna sheria ya kutumia nguvu pale ambako kuna mkusanyiko usiokuwa wa
halali pindi raia wanapokaidi kutawanyika kwa hiari hivyo hakuna shaka
kauli ya Waziri Mkuu ililenga hivyo.
Hata
hivyo, alisema hajapata taarifa za LHRC kumshtaki Waziri Mkuu
kimaandishi na kwamba akizipata atatoa ufafanuzi baada ya kuona lengo la
mashtaka.
Msimamo
Akizungumza
baada ya kufungua mashtaka hayo, Dk Bisimba alisema Waziri Mkuu anaweza
kushtakiwa kwa kuwa alizungumza kwa nafasi yake ya Waziri Mkuu na si
mbunge na kusisitiza kwamba hakuna aliye juu ya sheria na kudai kwamba
kauli hiyo ni kinyume cha Katiba.
Alisema
kuwa kila anayevunja Katiba lazima ashughulikiwe kisheria na kwamba
mahali pake ni mahakamani tu. Alisema kwa mujibu wa hati hiyo ya madai,
kauli na amri kama hizo zinapotolewa na kiongozi mwenye hadhi kama ya
mdaiwa wa kwanza (Waziri Mkuu) huchukuliwa kama sheria inayopaswa
kutekelezwa na wakala wa utekelezaji wa sheria kama vile polisi. Wadai
hao wanadai kuwa kwa ufahamu wao polisi wanaweza kuchukulia kauli hiyo
kama amri halali kutoka kwa mkubwa wao na hivyo kuwapiga na kuwatesa
watu wasio na hatia, kinyume cha Katiba.
Pia
wanadai wanatambua kuwa Ibara ya 100 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inatoa kinga kwa wabunge na uhuru wa maoni bungeni.
Hata hivyo, wanatambua kuwa Ibara ya 100 (2) ya Katiba hiyo
inawawajibisha wabunge wote chini ya masharti ya Katiba na kwamba kauli
aliyoitoa Waziri Mkuu Pinda inakiuka Ibara ya 12(12).
Hivyo wanaiomba Mahakama hiyo itamke kuwa kauli na amri hiyo aliyoitoa Pinda inavunja Katiba.
Mkurugenzi
wa taasisi inayofuatilia Mwenendo wa Bunge (Watch), Marcos Albania
alidai kwamba wamegundua kuwa kauli hiyo ya Pinda ni moja kati ya
matamko makubwa yanayovunja Katiba.
Alisema
mbali na shtaka hilo, kuna la pili dhidi ya Waziri Mkuu Pinda, ambalo
hawajalifikisha mahakamani ambalo pia linatokana na kauli hiyo aliyoitoa
bungeni kwamba: “Sasa wamechoka.”
SOURCE: CHAHALI.COM
No comments:
Post a Comment