Monday, December 24, 2012

Umoja wa waendesha pikipiki wa mkoa wa Mwanza waiomba Serikali iwape mafunzo na mkopo ili wanunue pikipiki.


Mkurugenzi Msaidizi kutoka  Idara ya Maendeleo ya Vijana  James Kajugusi  (kulia) akimkabidhi mwenyekiti wa Chama cha Umoja wa Waendesha Pikipiki mkoa wa Mwanza Makoye Bunoro Shilingi 50,000/= kwa ajili ya kuweka mafuta katika pikipiki za kitengo cha Polisi jamii pale wanapoenda kupambana na wahalifu.Umoja huo unawasaidia waendesha pikipiki  2034 kupata  leseni na mafunzo yaliyotolewa na Chuo cha VETA kwa gharama naafuu. 
Mkurugenzi Msaidizi kutoka  Idara ya Maendeleo ya Vijana  James Kajugusi  (kulia)  akiongea jambo hivi karibuni na viongozi wa umoja wa wapanda pikipiki wa mkoa wa Mwanza (hawapo pichani) alipowatembelea ofisini kwao eneo la Mlangommoja ili kuona shughuli zinazofanywa na umoja huo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Umoja huo Makoye Bunoro. 

Mdhibiti wa mali za chama ch Umoja  wa wapanda Pikipiki wa Mkoa wa Mwanza Faraji Abdalah akimwelezea Mkurugenzi Msaidizi kutoka  Idara ya Maendeleo ya Vijana  James Kajugusi  (kulia)  jinsi umoja huo ulivyoweza kuunda kitengo cha polisi jamii ambacho kinashirikiana na Jeshi la polisi katika kupambana na uhalifu. Katikati ni  Mwenyekiti wa Umoja huo Makoye Bunoro. 

Mwenyekiti wa Umoja  wa wapanda pikipiki wa mkoa wa Mwanza Makoye Bunoro (kushoto) akimweleza Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana  James Kajugusi  jinsi wapanda pikipiki wanavyohitaji kupata mafunzo na mikopo ya kununua pikipiki kutoka Serikalini ili waweze kujiajiri wenyewe na hivyo kujikwamua kiuchumi. (Picha na Anna Nkinda – Maelezo).

Na Anna Nkinda – Maelezo, Mwanza
Chama cha Umoja wa waendesha pikipiki wa mkoa wa Mwanza wameiomba Serikali kuwapa mafunzo ya uongozi pamoja na mikopo yenye masharti naafuu ili waweze kununua pikipiki zao binafsi na  kujiajiri wenyewe nahivyo kujiinua kiuchumi tofauti na ilivyo sasa kwani wengi wao wameajiriwa na hivyo kuwatajirisha waajiri wao.
Waendesha pikipiki hao ambao wengi wao ni vijana wametoa ombi hilo hivi karibuni wakati wakiongea na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana  James Kajugusi  wakati alipowatembelea ofisini kwao maeneo ya Mlango mmoja jijini Mwanza ili kuona shughuli zinazofanywa na umoja huo.

Akiongea kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Umoja huo Makoye Bunoro alisema kuwa kuna makampuni yanayokopesha pikipiki kwa riba kubwa jambo linasababisha mkopaji kuchukua  muda mrefu wa kulipa deni na kutokupata faida na kuyaomba makampuni hayo yakopeshe kwa riba ndogo ila nao wapate faida.

“Tatizo kubwa linalowakabili waendesha pikipiki ni kutokuwa na elimu, kama Serikali itatoa mafunzo kwa waendesha na wapanda pikipiki wote ajali za barabarani zitapungua kwa kiasi kikubwa kwani ajali nyingi zinatokana  na kutoelewa sheria za usalama barabarani kwa watumiaji wa vyombo hivyo”, alisema Bunoro .

Aliendelea kusema kuwa chama hicho  kinasimamia upatikanaji wa leseni, hadi sasa  waendesha pikipiki 2034 ambao ni wanachama na siyo wanachama wameshapata leseni pamoja na mafunzo yaliyotolewa na Chuo cha ufundi VETA  kwa gharama naafuu jambo ambalo limeweza kupunguza kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani zinazotokana na waendesha pikipiki katika  mkoa huo.

Wilaya ya Magu waliopata mafunzo na leseni ni 190, Sengerema 172, Misungwi 57, Ukerewe 106, Kwimba 28, Nyamagana na Ilemela 1484.
Bunora alisema,  “Ndani ya Chama chetu kuna kitengo cha Polisi Jamii ambacho kimekuwa kikipambana na matukio ya uhalifu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na tumeweza kuwakamata wahalifu ambao walishindikana na wengine walikuwa wanatafutwa kwa muda mrefu”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Kajugusi aliwataka vijana hao kuimarisha umoja wao na kutokubali kutumiwa na makundi ya watu kwa manufaa ya watu hao kwani vijana wananguvu za kutosha hivyo watu wengi wanapenda kuwatumia, bali wao watumie nguvu zao kutafuta ajira ambazo zitawainua kiuchumi  na kuleta maendeleo ya nchi yao.  
Alisema kuwa Serikali iliamua kuruhusu pikipiki kuwa chombo cha kuendesha abiria ili zisaidie katika masuala ya usafirishaji na kuongeza fursa ya upatikanaji wa ajira binafsi kwa vijana ili waweze kujiajiri wao wenyewe hivyo watambue kuwa biashara wanayoifanya ni halali jambo la muhimu ni kufuata  sheria zilizopo.

Kajugusi alisema, “Ninachowashauri muanzishe chama cha Kuweka Akiba na Kukopa  (SACCOS)  yenu ambayo itawawezesha kupata mkopo kirahisi kwani hivi sasa kuna fedha za mkopo wa mfuko wa vijana ambazo kupitia Halmashauri za wilaya zimewasaidia vijana wengi hapa nchini nanyi kama vijana mnastahili kupata fedha hizi”.
Alimalizia kwa kusema kuwa Idara ya vijana kwa kupitia vituo vyake vya kuwajengea uwezo vijana itaangalia  uwezekano wa kutoa mafunzo  kwa viongozi wa wapanda pikipiki wa wilaya ili wakawafundishe wenzao.

Umoja huo ulianzishwa mwezi wa pili mwaka 2011  na unajumla ya wanachama waliosajiliwa 1034 kutoka wilaya za Nyamagana 484, Ilemela 204, Sengerema 87, Ukerewe 51, Magu 123, Misungwi 57 na  Kwimba 28.

via mo blog
MWARICK JAPHET MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment