Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
(kushoto) akiangalia kahawa iliyolimwa na Ibrahim Mulokozi (kulia)
ambaye ni mkazi wa kijiji cha Ibwera wilayani Bukoba aliyenufaika na
mkopo wa shilingi laki nne kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana. Waziri
Dk. Mukangara alilitembelea shamba hilo la kahawa na migomba jana ili
kuona fedha za mkopo walizozipata vijana kutoka SACCOS ya Ibwera
zimewanufaishaje kimaisha.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
(kushoto) akimuangalia samaki mwenye umri wa miezi mitatu anayefugwa
katika bwawa la Kikundi cha Msifuni kilichopo kijiji cha Kemondo
wilayani Bukoba ambacho kilipata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana. Waziri Dk. Mukangara alilitembelea bwawa hilo jana ili kuona
fedha za mkopo walizozipata vijana kupitia mfuko wa Halmashauri
nimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (wa tatu
kulia) akiangalia jana nyavu za kuvulia samaki za Kikundi cha Msifuni
kilichopo katika kijiji cha Kemondo wilayani Bukoba ambacho kilipata
mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya vijana na kuanzisha mradi wa bwawa la
samaki. Kushoto ni Katibu wa kikundi hicho Johanes Joel.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
(kushoto) akipokea taarifa ya SACCOS ya Ibwera iliyopo wilayani Bukoba
kutoka kwa Benedicta Peter ambaye ni katibu msaidizi. SACCOS hiyo
ilipata mkopo wa shilingi milioni tano kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara
akiangalia shamba la kahawa na migomba la mkazi wa kijiji cha Ibwera
wilayani Bukoba Ibrahim Mulokozi (haupo pichani) wakati alipolitembelea
jana ili kuona fedha za mkopo wa mfuko wa vijana alizozipata kupitia
SACCOS ya Ibwera zimemnufaishaje kimaisha. Kushoto ni Mkurugenzi
Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Vijana James Kajugusi.
Waziri
wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk. Fenella Mukangara (wanne
kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wanachama wa SACCOS ya Ibwera
na viongozi wa wilaya ya Bukoba wakati alipowatembelea jana ili kuona
fedha walizopata kutoka mfuko wa waendeleo ya vijana zilivyoweza
kuwasaidia vijana kujikwamua kimaisha. (Picha na Anna Nkinda – Maelezo).
Na Anna Nkinda – Maelezo, Kagera
Serikali
imeombwa kuongeza kiasi cha mkopo kinachotoa kwa vijana kupitia mfuko
wa maendeleo wa vijana na Halmashauri za wilaya kwani kiwango
kinachotolewa kwa sasa cha shilingi milioni tano kwa vyama vya Kuweka
Akiba na Kukopa (SACCOS) ni kidogo ukilinganisha na mahitaji ya mkopo
huo.
Ombi
hilo limetolewa jana na baadhi ya vijana waliopata mkopo huo kupitia
SACCOS ya Ibwera na halmashauri ya wilaya ya Bukoba wakati wakiongea kwa
nyakati tofauti na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk.
Fenella Mukangara alipotembelea wilaya hiyo ili kuona jinsi fedha hizo
zilivyoweza kuwasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Vijana
hao walisema kuwa fedha za mkopo walizozipata zimewasaidia kujiinua
kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuajiri vijana wenzao, kupanua mitaji ya
biashara zao, kulipa karo za shule za watoto wao na kujikwamua kimaisha
tofauti na ilvyokuwa awali kaba hawajapata mkopo na kufanya shughuli za
ujasiriamali.
Kwa
upande wake mkazi wa kijiji cha Ibwera Ibrahim Mulokozi ambaye alipata
mkopo wa shilingi laki nne kupitia SACCOS ya kijiji hicho alisema kuwa
ameweza kununua matandazo na kulipa wasaidizi wanaohudumia shamba lake
la migimba na kahawa ambalo ni la mfano kwa vijana na wazee wanaotoka
kata ya Ibwera, Mikoni na Nyakibimbili na kwenda kujifunza na kuchukua
miche ya migomba.
Alisema
kuwa anakabiliwa na changamoto za kutokuwa na fedha za kuendeleza
shughuli za kilimo, kutoka na mbolea ya kutosha ya kurutubisha shamba,
bei ya miche ya kahawa kupanda kutoka shilingi 50 hadi 500 kwa mche
mmoja, kuendelea kutumia jembe la mkono, kutokuwa na masoko ya uhakika
hasa soko la ndizi na magonjwa ya migomba.
Naye
katibu wa kikundi cha Msifuni Johanes Joel ambacho kilipata mkopo wa
shilingi milioni moja na laki tano kutoka Halmashauri ya wilaya ya
Bukoba alisema kuwa kikundi chao kinajishughulisha na kazi ya ukulima
wa samaki na walianza na bwawa moja na hivi sasa wana mabwawa matatu
na wanampango wa kuhakikisha kuwa kila mwanakikundi anakuwa na bwawa
lake.
“Changamoto
zinazotukabili ni kutokuwa na mtaji wa kutosha, wanachama kutokuwa na
elimu ya kuendesha na kusimamia au kutunza miradi na kufanyiwa hujuma
kwa mradi wetu wa samaki ikiwa ni pamoja na kuibiwa na kuharibiwa kwa
mabwawa hasa nyakati za usiku na watu wasiopenda kufanya kazi za
maendeleo”, allisema Joel.
Kwa
upande wake waziri Dk. Mukangara aliwataka vijana wa kijiji hicho
kufanya kazi kwa kujituma na kujiunga katika vikundi vya maendeleo jambo
ambalo litawafanya waweze kupata mikopo kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana na halmashauri ya wilaya na hivyo kuweza kujishughulisha na
kazi za upandaji wa miti, kilimo cha samaki na ufugaji wa ng’ombe wa
maziwa na nyuki.
Dk.
Mukangara alisema, “Vijana ni lazima mfanye kazi na kuachana na tabia
ya uvivu, kufanya kazi si lazima uajiriwe bali unaweza kujiajiri wewe
mwenyewe kama hapa Ibwera kunahali ya hewa nzuri na milima mingi haina
miti mnaweza kuwa na mradi wa kupanda miti na kufuga nyuki ambao
watawapatia asali na mkiiuza mtapata fedha nahivyo kujikwamua
kiuchumi”.
Kwa
upande wa mafunzo ya ujasiriamali waziri Dk. Mukangara alisema kuwa
wizara yake inavituo vya kuwajenge uwezo vijana hivyo basi kama wahusika
ambao ni vijana watakuwa tayari kupata mafunzo ya ushirika na mafunzo
mengine kama ya uongozi, stadi za maisha watayapata na yatawasaidia
katika maisha yao.
Waziri
Dk. Mukangara alikuwa mkoani Kagera kwa ajili ya kukagua SACCOS na
vikundi vya vijana vilivyopata mkopo kutoka mfuko wa maendeleo ya
vijana ili kuona fedha hizo zimewasaidiaje vijana kujikwamua kiuchumi.
Katika wilaya ya Bukoba alilitembelea shamba la mfano la kahawa na
migomba, kikundi cha burudani cha Rugazi na shamba la samaki la
kikundi cha Msifuni.
mo blog