Wednesday, September 7, 2016

Ujenzi nyumba za Magomeni Kota kukamilika mwakani


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 06 Septemba, 2016 amewatembelea Wakazi wa Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam ambao nyumba walizokuwa wakiishi katika eneo hilo zilivunjwa mwaka 2012 kwa makubaliano ya kujengwa nyumba za kisasa na kuwaahidi kuwa Serikali itaanza kujenga nyumba hizo katika kipindi cha Miezi miwili kuanzia sasa.


Rais Magufuli amesema ujenzi wa nyumba hizo utakamilika katika kipindi cha mwaka mmoja na baada ya hapo Wakazi wote 644 walioondolewa kupisha ujenzi wa nyumba za kisasa watapatiwa nyumba za kuishi na kwamba wataishi katika nyumba hizo kwa muda wa miaka mitano bila kulipa pango na baada ya muda huo kuisha wataandaliwa utaratibu wa kila mmoja kuuziwa nyumba anayoishi.


"Nakwenda kutoa pesa Mwezi huu, ili Mkandarasi atakayeteuliwa aanze kujenga nyumba za wakazi wote 644, wakati wanapojenga hayo majengo ya wakazi 644, ujenzi utaendelea pia katika maeneo mengine, ili kusudi kama yanajengwa maduka makubwa (Shopping Malls) au zinajengwa nyumba zingine za wananchi wanaohangaika nao tuwalete hapa.


"Nataka katika miji yetu ya Tanzania tuanze kupambana na makazi ya wananchi, tuwe tunajenga nyumba ili hata hawa masikini wa Tanzania waweze kufaidi kukaa kwenye ghorofa" Amesema Rais Magufuli.


Aidha, Dkt. Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na namna tatizo la wakazi wa Magomeni Kota lilivyoshughulikiwa na amewaahidi kuwa Serikali yake itahakikisha wananchi hao hawasumbuliwi tena.


Pamoja na hatua alizochukua kwa wakazi wa Magomeni Kota ambao nyaraka zimeonesha walikuwa wakiishi katika Nyumba za Shirika la Nyumba (NHC), Rais Magufuli ameagiza maeneo yote katika mikoa 20 hapa nchini yenye nyumba za kuishi za NHC kama lilivyo eneo hilo yatwaliwe na Serikali na kwamba Serikali itatoa maelekezo ya namna yatakavyotumika ama kuendelezwa.


Pamoja na kumpongeza kwa kazi nzuri anazofanya, Rais Magufuli amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Shirika na Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Neemia Mchechu Kyando kuwaondoa wapangaji ambao ni wadaiwa sugu wa pango zikiwemo Taasisi za Serikali ambazo amezipa siku saba kuwa zimelipa madeni yao.


"Wale wapangaji wote lazima walipe madeni yao, nimetoa maagizo leo, wapangaji wote wa Serikali, Wizara ya Ujenzi, Wizara gani kule... ndani ya siku saba lazima wawe wameshalipa madeni yao wasipolipa endelea kuwatoa nje.


"Endelea hivyo hivyo usiogope kumtoa nje mtu yeyote, awe amepangishwa ni wa CCM mtoe nje, awe wa UKAWA mtoe nje, awe Serikali mtoe nje, awe Waziri Mtoe nje, mpangaji huyo awe ni Rais mtoe nje, ni lazima upate pesa zitakazowezesha kuendesha Shirika la Nyumba la Taifa" Amesisistiza Rais Magufuli.


Wakati huo huo, Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa chuo hicho alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho tarehe 02 Juni, 2016.


Jumla ya majengo 20 yenye ghorofa nne kila moja yanajengwa katika eneo hilo la mashariki mwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na yatakapokamilika tarehe 31 Desemba, 2016 yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 3,840 kati ya wanachuo 7,000 wanaolazimika kupanga vyumba vya kuishi mitaani kutokana na kukosa nafasi katika mabweni ya chuo yaliyopo.


Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Vijana walioajiriwa katika kazi za ujenzi wa majengo hayo Rais Magufuli amepongeza moyo wa uzalendo waliouonesha kwa kufanya kazi usiku na mchana na amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga kuendelea kuwatumia vijana hao katika miradi mingine ambayo Serikali itaitekeleza kwa kutumia TBA.

TBA ikitumia wataalamu na Vijana wa Kitanzania itatumia Shilingi Bilioni 10 kukamilisha ujenzi huo ikilinganishwa na endapo ingetumia Wakandarasi ambao walitaka kulipwa kati ya Shilingi Bilioni 50 na Bilioni 100.


Rais Magufuli ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuacha kuingia mikataba mingine na wafanyabiashara wanaotumia maeneo ya chuo hicho kujenga majengo ya kibiashara na badala yake amesema Serikali itaendelea kutafuta namna ya kulimaliza tatizo la mabweni kwa wanafunzi wa chuo hicho na vyuo vingine hapa nchini. 

MWARICK JAPHET MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

No comments:

Post a Comment