Siku chache baada ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litoe nje vitu vya
mmiliki wa Mbowe Hotels Limited, Freeman Mbowe kwa kile kilichoelezwa
kushindwa kulipa kodi ya pango iliyofikia Sh bilioni 1.172 , Rais Dk.
John Magufuli amempongeza Mkurugenzi wa Shirika hilo, Nehemia Mchechu
kwa hatua hiyo.
Pamoja na hali hiyo ametoa siku saba kufukuzwa kwa wapangaji wote wa NHC
watakaoshindwa kulipa kodi ya pango, zikiwemo wizara, taasisi za
Serikali, watu binafsi na watumishi wa umma.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na waliokuwa
wakazi wa Magomeni Kota, Rais Dk. Magufuli, alisema hatua
zinazochukuliwa na Mchechu zitasaidia upatikanaji wa fedha za kuwekeza
kwenye miradi mipya.
“Nakupongeza kwa hatua unazoendelea kuchukua. Wale wapangaji wote ni
lazima walipe madeni yao, nimetoa maagizo leo (jana) wapangaji wote wa
Serikali, Wizara ya Ujenzi, wizara gani kule ndani ya siku saba lazima
wawe wameshalipa madeni yao,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Wasipolipa endelea kuwatoa nje kama ulivyomtoa yule jamaa (Mbowe),”
alisema na kusababisha watu kushangilia huku wakiangua vicheko.
“Endelea hivyo hivyo usiogope kumtoa nje mtu yeyote. Awe amepangishwa ni
wa CCM mtoe nje, awe ni wa Ukawa mtoe nje, awe mtumishi wa Serikali
mtoe nje, awe mtumishi huyo ni waziri mtoe nje, awe ni Rais mtoe nje,”
alisema Rais Magufuli.
Alisema anashangaa kuona watumishi wa Serikali wakishindwa kulipa madeni
ya kodi za pango wakati kila siku wanaomba safari za nje huku
wakilipana posho.
“Ukipanga na ukashindwa kulipa kodi jiandae kuondoka. Nataka uendelee
kuwatoa na nakueleza kweli Nehemia sitanii ‘take it from me and I am
very serious’ (nisikilize mimi sifanyi mzaha) ” alisisitiza.
Alisema madeni hayo yangekusanywa yangelisaidia shirika hilo kuwekeza
katika maeneo kama la Magomeni Kota ambalo limekaa kwa muda mrefu bila
kuendelezwa.
“Inawezekana ungekuwa na hizo fedha ungeshajenga katika eneo hili kuliko
kuanza kumtafuta mwekezaji kwa ujanjaujanja. Haiwezekani eneo kama hili
(Magomeni Kota) la ekari 33 unazitoa hivi hivi na ni mali ya Serikali,
“Afadhali umtoe mke wako umpe mzaramo mtani wangu akae naye,” alisema Rais Magufuli huku wananchi wakiangua kicheko.
Alimsisitizia Mchechu kuharakisha kuzitoa wizara zinazodaiwa kwenye
majengo yake ili ziharakishe kwenda kujenga Dodoma yaliko makao makuu ya
nchi.
Awali Rais Magufuli, alisema alibaini ukweli kuhusu eneo hilo kwamba
lilitaka kuuzwa kwa mwekezaji kinyemela na kuwaacha bila kitu wakazi
hao.
VIA Mtanzania
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment