Na, Shushu Joel,BUSEGA
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi
Masanza katika Kijiji cha Mitindu Kata ya Kiloleli, Wilaya ya Busega, Mkoani
Simiyu, wanalazimika kusomea kwenye mti kutokana na upungufu wa madarasa.
Aidha upungufu huo wa madarasa unawalazimu
wanafunzi wengine kusomea juani katika madarasa mawili ambayo hayajapauliwa
licha kufikia hatua hiyo miaka miwili iliyopita.
Shule hiyo ilianzishwa tangu mwaka 2006
lakini mpaka sasa haina hata nyumba moja ya walimu.
|
Wanafunzi wa shule ya msingi masanza wakiwa darasani |
Akizungumza na NIPASHE mwalimu mkuu wa shule
hiyo Vedasto Chibuga amesema kutokana na
uwepo wa changamoto hizo kunapelekea idadi kubwa ya wanafunzi kusomea kwenye
darasa la vyumba viwili ambalo halijaezekwa, huku wengine wakisomea chini miti.
Chibuga aliongeza kuwa wanaosomea kwenye
darasa hilo ni wanafunzi wa awali,darasa la sita na darasa la tatu, lakini
ikifika majira ya saa tano asubuhi hulazimika kuthitisha vipindi kutokana na
jua kali na kwenda kuwachanganya na wananfunzi madarasa mengine.
“Sera ya elimu inasema kuwa kila chumba
wasome wanafunzi 45 lakini hapa kwangu mkondo mmoja wanasoma wanafunzi
wasiopungua 100 kutokana na changamoto
hizo za uhaba wa vyumba vya madara”.
Aidha Chibuka alisema kuwa serikali ndio ya
kulaumiwa kwani wananchi wao walitimiza wajibu wao wa kuchangishana kwa ajili
ya ujenzi wa boma hilo tangu mwaka 2013.
Kwa muji mwalimu mkuu huyo, hali inawafanya
walimu kukata tamaa hali inayopelekea wanafunzi kutofanya vizuri kwenye matokeo
ya mitihani ya kitaifa kutokana na mazingira magumu ya kufundishia.
Mmoja wa wazazi wa wanafunzi katika shule
hiyo, Mikwanga Yona, alisema kuwa ni aibu kwa serikali kushindwa kupaua jengo
hilo lililojengwa kwa nguvu za wananchi, na kwamba hali hiyo inaweza kufanya
wananchi kukata tamaa kuchangia maendeleo katika maeneo yao kwa kukatishwa
tamaa na serikali kwa kushindwa kuunga mkono jitihada zao.
|
Wanafunzi wakiwa darasani na mwalimu wao akiwafundisha |
Ofisa Elimu Kata ya Kiloleli John Mayunga
amethibitisha kuwepo kwa hali hiyo, na kwamba jambo hilo wamelifikisha katika
kikao cha maendeleo ya kata ambacho mwenyekiti wake huwa diwani wa kata husika,
na kuongeza kuwa pengine serikali inalifanyia hivyo kwa kuwa walishaliwasilisha
katika ngazi ya halmashauri.
>>>>>>>>>>MWISHO>>>>>>