Wednesday, September 7, 2016

MAFUTA YASHUKA BEI


Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji na Mafuta (Ewura), imetangaza kushuka bei ya mafuta ya aina zote kwa jumla na rejareja.


Bei hizo mpya ya mafuta zimeshuka katika mikoa yote isipokuwa Mkoa wa Tanga, hasa kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa.



Taarifa ya Ewura jana ilisema bei hizo zimeshuka ikilinganishwa na toleo la bei za mafuta hayo lililopita la Agosti 3, mwaka huu.



Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema katika toleo hilo, bei ya rejareja kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa imepungua kwa viwango tofauti.



Alisema kwa petroli imeshuka kwa Sh 65, dizeli Sh 63 na mafuta ya taa Sh 86.



“Bei ya jumla imepungua ambako kwa petroli ni Sh 65.31, dizeli Sh 63.39 na mafuta ya taa Sh 85.93,” alisema.



Ngamlagosi alisema kushuka kwa bei ya petroli katika soko la dunia na kupungua kwa gharama za usafarishaji/uletaji wa mafuta hayo nchini, ndizo sababu kuu zilizochangia kushuka kwa bei ya mafuta katika soko la ndani nchini.



“Bei ya jumla na rejareja kwa petroli na dizeli katika Mkoa wa Tanga imeongezeka kidogo ikilinganishwa na toleo la bei za mafuta hayo lililopita la Agosti 3, 2016.



“Katika toleo hili, bei ya rejareja kwa petroli na dizeli imeongezeka kwa viwango ambavyo petroli ni Sh 50 na dizeli Sh 19. Kwa kulinganisha na matoleo haya mawili, bei ya jumla imeongezeka.



“Petroli Sh 49.61 kwa lita sawa na asilimia 2.80 na dizeli Sh 18.57 kwa lita sawa na asilimia 1.1.



“Ongezeko hili la bei limechangiwa kwa kiasi kikubwa na kupokea mafuta mapya (petroli na dizeli) ndani ya Agosti 2016, ambayo yalitarajiwa kupokewa Julai 2016 na pia kutokupokea mafuta mapya kutoka katika meli ya MT. Nevaska Lady ndani ya Agosti mwaka huu,” alisema Ngamlagosi.



Hata hivyo, alisema mamlaka hiyo inawakumbusha wananchi kwamba bei kikomo ya mafuta kwa eneo husika, pia inapatikana kupitia simu zao za mkononi kwa kupiga namba *152*00# na kufuata maelekezo.



Alisema huduma hiyo hutolewa bure na inapatikana kupitia mitandao yote ya simu za mkononi nchini.
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

JPM atoa siku saba kwa wadaiwa sugu NHC


Siku chache baada ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) litoe nje vitu vya mmiliki wa Mbowe Hotels Limited, Freeman Mbowe kwa kile kilichoelezwa kushindwa kulipa kodi ya pango iliyofikia Sh bilioni 1.172 , Rais Dk. John Magufuli amempongeza Mkurugenzi wa Shirika hilo, Nehemia Mchechu kwa hatua hiyo.

Pamoja na hali hiyo ametoa siku saba kufukuzwa kwa wapangaji wote wa NHC watakaoshindwa kulipa kodi ya pango, zikiwemo wizara, taasisi za Serikali, watu binafsi na watumishi wa umma.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota, Rais Dk. Magufuli, alisema hatua zinazochukuliwa na Mchechu zitasaidia upatikanaji wa fedha za kuwekeza kwenye miradi mipya.


“Nakupongeza kwa hatua unazoendelea kuchukua. Wale wapangaji wote ni lazima walipe madeni yao, nimetoa maagizo leo (jana) wapangaji wote wa Serikali, Wizara ya Ujenzi, wizara gani kule ndani ya siku saba lazima wawe wameshalipa madeni yao,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:


“Wasipolipa endelea kuwatoa nje kama ulivyomtoa yule jamaa (Mbowe),” alisema na kusababisha watu kushangilia huku wakiangua vicheko.


“Endelea hivyo hivyo usiogope kumtoa nje mtu yeyote. Awe amepangishwa ni wa CCM mtoe nje, awe ni wa Ukawa mtoe nje, awe mtumishi wa Serikali mtoe nje, awe mtumishi huyo ni waziri mtoe nje, awe ni Rais mtoe nje,” alisema Rais Magufuli.


Alisema anashangaa kuona watumishi wa Serikali wakishindwa kulipa madeni ya kodi za pango wakati kila siku wanaomba safari za nje huku wakilipana posho.


“Ukipanga na ukashindwa kulipa kodi jiandae kuondoka. Nataka uendelee kuwatoa na nakueleza kweli Nehemia sitanii ‘take it from me and I am very serious’ (nisikilize mimi sifanyi mzaha) ” alisisitiza.


Alisema madeni hayo yangekusanywa yangelisaidia shirika hilo kuwekeza katika maeneo kama la Magomeni Kota ambalo limekaa kwa muda mrefu bila kuendelezwa.


“Inawezekana ungekuwa na hizo fedha ungeshajenga katika eneo hili kuliko kuanza kumtafuta mwekezaji kwa ujanjaujanja. Haiwezekani eneo kama hili (Magomeni Kota) la ekari 33 unazitoa hivi hivi na ni mali ya Serikali,


“Afadhali umtoe mke wako umpe mzaramo mtani wangu akae naye,” alisema Rais Magufuli huku wananchi wakiangua kicheko.

Alimsisitizia Mchechu kuharakisha kuzitoa wizara zinazodaiwa kwenye majengo yake ili ziharakishe kwenda kujenga Dodoma yaliko makao makuu ya nchi.


Awali Rais Magufuli, alisema alibaini ukweli kuhusu eneo hilo kwamba lilitaka kuuzwa kwa mwekezaji kinyemela na kuwaacha bila kitu wakazi hao.


VIA Mtanzania
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

Darasa la saba waanza mitihani leo



WATAHINIWA 795,761 wanatarajia kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) unaofanyika leo na kesho nchini kote.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk Charles Msonde alisema wanafunzi 372,883 ambao ni sawa na asilimia 46.86 ni wavulana na wasichana ni 422,878 ambao ni asilimia 53.14.


Mwaka 2015 watahiniwa waliosajiliwa kufanya mtihani walikuwa 775,729 huku 763,602 ndio waliofanya mtihani huo na wanafunzi 518,034 walifaulu.


Dk Msonde alisema watahiniwa 765,097 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 30,664 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia. Masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa.


Alisema watahiniwa wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani ni 95 wakiwemo wavulana 57 na wasichana 38 wakati wale wenye uoni hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa ni 810 ambao kati yao wavulana ni 402 na wasichana ni 408.


“Maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika kiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, fomu maalum za kujibia mtihani na nyaraka zote muhimu katika halmashauri na manispaa zote nchini,” alisema Dk Msonde.


Aidha, Dk Msonde alitoa mwito kwa kamati za mitihani za mikoa na halmashauri kuhakikisha taratibu za mitihani ya Taifa zinazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya vituo vya mitihani yanakuwa salama, tulivu na kuzuia mianya ya udanganyifu.


“Wasimamizi wanatakiwa kusimamia kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu. Nawaaasa kujiepusha na vitendo vya udanganyifu kwani Baraza litachukua hatua kali kwa yeyote yule atakayebainika kukiuka taratibu za uendeshaji wa mitihani ya Taifa,” alieleza.
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

Ujenzi nyumba za Magomeni Kota kukamilika mwakani


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli jana tarehe 06 Septemba, 2016 amewatembelea Wakazi wa Magomeni Kota Jijini Dar es Salaam ambao nyumba walizokuwa wakiishi katika eneo hilo zilivunjwa mwaka 2012 kwa makubaliano ya kujengwa nyumba za kisasa na kuwaahidi kuwa Serikali itaanza kujenga nyumba hizo katika kipindi cha Miezi miwili kuanzia sasa.


Rais Magufuli amesema ujenzi wa nyumba hizo utakamilika katika kipindi cha mwaka mmoja na baada ya hapo Wakazi wote 644 walioondolewa kupisha ujenzi wa nyumba za kisasa watapatiwa nyumba za kuishi na kwamba wataishi katika nyumba hizo kwa muda wa miaka mitano bila kulipa pango na baada ya muda huo kuisha wataandaliwa utaratibu wa kila mmoja kuuziwa nyumba anayoishi.


"Nakwenda kutoa pesa Mwezi huu, ili Mkandarasi atakayeteuliwa aanze kujenga nyumba za wakazi wote 644, wakati wanapojenga hayo majengo ya wakazi 644, ujenzi utaendelea pia katika maeneo mengine, ili kusudi kama yanajengwa maduka makubwa (Shopping Malls) au zinajengwa nyumba zingine za wananchi wanaohangaika nao tuwalete hapa.


"Nataka katika miji yetu ya Tanzania tuanze kupambana na makazi ya wananchi, tuwe tunajenga nyumba ili hata hawa masikini wa Tanzania waweze kufaidi kukaa kwenye ghorofa" Amesema Rais Magufuli.


Aidha, Dkt. Magufuli ameelezea kusikitishwa kwake na namna tatizo la wakazi wa Magomeni Kota lilivyoshughulikiwa na amewaahidi kuwa Serikali yake itahakikisha wananchi hao hawasumbuliwi tena.


Pamoja na hatua alizochukua kwa wakazi wa Magomeni Kota ambao nyaraka zimeonesha walikuwa wakiishi katika Nyumba za Shirika la Nyumba (NHC), Rais Magufuli ameagiza maeneo yote katika mikoa 20 hapa nchini yenye nyumba za kuishi za NHC kama lilivyo eneo hilo yatwaliwe na Serikali na kwamba Serikali itatoa maelekezo ya namna yatakavyotumika ama kuendelezwa.


Pamoja na kumpongeza kwa kazi nzuri anazofanya, Rais Magufuli amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Shirika na Nyumba la Taifa (NHC) Bw. Neemia Mchechu Kyando kuwaondoa wapangaji ambao ni wadaiwa sugu wa pango zikiwemo Taasisi za Serikali ambazo amezipa siku saba kuwa zimelipa madeni yao.


"Wale wapangaji wote lazima walipe madeni yao, nimetoa maagizo leo, wapangaji wote wa Serikali, Wizara ya Ujenzi, Wizara gani kule... ndani ya siku saba lazima wawe wameshalipa madeni yao wasipolipa endelea kuwatoa nje.


"Endelea hivyo hivyo usiogope kumtoa nje mtu yeyote, awe amepangishwa ni wa CCM mtoe nje, awe wa UKAWA mtoe nje, awe Serikali mtoe nje, awe Waziri Mtoe nje, mpangaji huyo awe ni Rais mtoe nje, ni lazima upate pesa zitakazowezesha kuendesha Shirika la Nyumba la Taifa" Amesisistiza Rais Magufuli.


Wakati huo huo, Rais Magufuli amekagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa kwa chuo hicho alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa maktaba ya kisasa ya chuo hicho tarehe 02 Juni, 2016.


Jumla ya majengo 20 yenye ghorofa nne kila moja yanajengwa katika eneo hilo la mashariki mwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na yatakapokamilika tarehe 31 Desemba, 2016 yatakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 3,840 kati ya wanachuo 7,000 wanaolazimika kupanga vyumba vya kuishi mitaani kutokana na kukosa nafasi katika mabweni ya chuo yaliyopo.


Akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na Vijana walioajiriwa katika kazi za ujenzi wa majengo hayo Rais Magufuli amepongeza moyo wa uzalendo waliouonesha kwa kufanya kazi usiku na mchana na amemuagiza Mtendaji Mkuu wa TBA Elius Mwakalinga kuendelea kuwatumia vijana hao katika miradi mingine ambayo Serikali itaitekeleza kwa kutumia TBA.

TBA ikitumia wataalamu na Vijana wa Kitanzania itatumia Shilingi Bilioni 10 kukamilisha ujenzi huo ikilinganishwa na endapo ingetumia Wakandarasi ambao walitaka kulipwa kati ya Shilingi Bilioni 50 na Bilioni 100.


Rais Magufuli ameutaka uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuacha kuingia mikataba mingine na wafanyabiashara wanaotumia maeneo ya chuo hicho kujenga majengo ya kibiashara na badala yake amesema Serikali itaendelea kutafuta namna ya kulimaliza tatizo la mabweni kwa wanafunzi wa chuo hicho na vyuo vingine hapa nchini. 

MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

Friday, September 2, 2016

ORODHA YA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO AWAMU YA PILI (SECOND SELECTION) KWA MWAKA 2016


TAARIFA KWA UMMA


OR-TAMISEMI inatangaza majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya Pili (Second Selection) kwa mwaka 2016. Jumla ya wanafunzi 3,918 wakiwemo wasichana 2,413 na wavulana 1,505 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi na wanafunzi ambao hawakuripoti awamu ya kwanza. 

Kati ya wanafunzi waliochaguliwa 1,864 wakiwemo wasichana 1,099 na wavulana 765 sawa na asilimia 47.58 watajiunga na masomo ya Sayansi na Hisabati; na wanafunzi 2,054 wakiwemo wasichana 1,314 na wavulana 740 sawa na asilimia 52.42 wamechaguliwa kusoma masomo ya Sanaa na Biashara. 

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili mwaka 2015 wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangwa kwa wakati. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya tangazo hili atakuwa amepoteza nafasi hii. 

Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili mwaka 2016 inapatikana kwenye tovuti ya OR-TAMISEMI ya www.tamisemi.go.tz

Imetolewa na Katibu Mkuu,
OR-TAMISEMI

Tumia link hii kupata matokeo :
>> Waliochaguliwa kidato cha tano awamu ya pili 2016


Link ya Matokeo ya awali : >> Waliochaguliwa kidato cha tano na vyuo vya ufundi 2016

MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.