Tuesday, September 11, 2012

WANAHABARI WAMTIMUA WAZIRI NCHIMBI KATIKA MAANDAMANO YAO.


Katibu wa Jukwaa la Wahariri Bw. Nevil Meena akiongea kwa uchungu mbele ya wanahabari wenzake ambapo pamoja na maazimio mengine wametangaza kutoandika habari zinazohusiana na jeshi la polisi kwa siku 40. 
Na Datus Boniface.

Wakiwa katika nyuso za huzuni kubwa ya kuondokewa na mwenzao ambaye aliuawa kwa kupigwa na bomu, kundi la Wanahabari wao wamemtimua Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Emmanuel Nchimbi kutokana na kuwaingilia kwenye maandamano yao.

Wanahabari kote nchini leo wamefanya maandamano ya amani kwa lengo la Kulaani mauaji ya mwenzao wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.

Kufukuzwa na kuzomewa kwa Waziri Nchimbi kumekuja baada ya kugundulika kuwa ameingilia maandamano kwa lengo la kuyapokea bila kupewa mwaliko.

Kutokana na zomea zomea hiyo ya wanahabari hao dhidi ya Waziri Nchimbi hali ilionekana kuwa si shwari na kupelekea waziri huyo kuondolewa na rais wa UTPC Keneth Simbaya na viongozi wengine wakiwemo askari polisi.

Akizungumza na kundi la waandishi Katibu wa Jukwaa la Jukwaa la wahariri (TEF) Neville Meena amesema “Hatuna ugomvi na Waziri Nchimbi kwani ni mwenzetu, rafiki yetu, ila leo hana vazi la msiba”

Mara baada ya kuondoka bila kupenda Waziri Nchimbi, hali ya utulivu ilikuwa kama kawaida na shughuli zingine ziliendelea kama ilivyopangwa.


VIA . MO BLOG
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

Thursday, September 6, 2012

KUUAWA KWA MWANDISHI IRINGA: CCM YATAKA UCHUNGUZI UFANYIKE KWA UMAKINI NA WELEDI MKUBWA.


Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Nape Nnauye.

-Yataka usichukue muda mrefu
-Yataka ubaini pia mazingira ya kuuawa mwandishi huyo.
-Yatoa pole kwa wafiwa, Wanahabari na Watanzania.

CCM imevitaka vyombo na tume zilizoundwa kuhusiana na kifo cha mwandishi wa habari Daudi Mwangosi, vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini kila kitu ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira yaliyosabaisha kipigo  hadi kufa mwandishi huyo.

Aidha imetaka uchunguzi usichukue muda mrefu ili ukweli kuhusiana na kadhia hiyo ujulikane mapema na hatua zichukuliwe kwa kila atakayebainika kuwa sababu au chanzo cha vurugu na kifo cha mwandishi huyo.

Aidha imesema imepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari watatu wa Polisi wakati wa vurugu hizo na kimetoa pole kwa wafiwa, wanahabari wote nchini na wote walioguswa na msiba huo kwa namna moja au nyingine.

Hayo yamesemwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye katika taarifa ya CCM kwa vyombo vya habari, leo jijini hapa, kuhusiana na sakata la vurugu hadi kifo cha mwandishi huyo, juzi mkoani Iringa.

“Itakumbukwa tarehe Septemba 2, 2012 katika operesheni za CHADEMA mkoani Iringa kulitokea vurugu zilizosababisha kuuawa kwa mwandishi wa habari mzoefu,nDaudi Mwangosi na kujeruhiwa vibaya kwa  polisi watatu wa kikosi cha kutuliza ghasia. Chama Cha Mapinduzi kimepokea kwa masikitiko makubwa sana taarifa za kifo hicho na kujeruhiwa kwa askari hao”, Nape alisema katika taarifa hiyo, na kuongeza:

“CCM inachukua nafasi hii kutoa pole kwa wafiwa, wanahabari nchini na wote walioguswa na msiba huu kwa namna moja au nyingine na tunatoa mwito kwa vyombo na tume mbalimbali zilizoundwa kuchunguza swala hili, vichunguze kwa umakini na weledi mkubwa ili kubaini yote – ikiwemo chanzo cha vurugu zilizotokea na mazingira ya kifo cha ndugu yetu”.

Alisema CCM  inasikitishwa na mfululizo wa matukio ya watu kupoteza maisha au kujeruhiwa katika mikutano na operesheni mbalimbali zinazoendeshwa na CHADEMA nchini hasa zile zilizofanyika kwa kukaidi amri halali za vyombo vya ulinzi na usalama.

Alikumbusha baadhi ya matukio hayo kuwa ni pamoja na lile la kuuawa kwa kada wa CCM Mkoani Singida, kuuawa kwa Ally Hassan mjini Morogoro na la juzi la kuuawa kwa Mwangosi Mjini Iringa, kujeruhiwa kwa askari polisi Iringa na matukio mengine mengi ambayo yametokea wakati CHADEMA wakiendesha operesheni zao mbalimbali nchini.

“Matukio haya si mazuri kutokea kwenye shughuli za Chama cha siasa. Kwakweli ni aibu, inayohitaji uwajibikaji,hata kama ni wa kisiasa. Inapotokea shughuli za chama chako zinasababisha kupotea kwa maisha ya watu kila unapozifanya na bado usitake kuwajibika, inahitaji roho ngumu na ujasiri wa aina yake” alisema Nape katika taarifa hiyo na kuongeza;
“Inakuwa mbaya zaidi pale vifo hivi vinaposababishwa na Chama hicho kutotii amri halali zilizotolewa kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi inayovipa pia uhalali  vyama vya siasa kuwepo na kuendesha shughuli zake kwa mujibu wa sheria”.

“Laiti Chama hicho kingesubiri siku chache zilizobakia kabla ya Sensa kuisha kabla ya kuendelea na mikutano yake ni dhahiri mauaji haya yasingetokea. Lakini kauli za kukebehi na uamuzi wa kukaidi amri ya Jeshi la Polisi na kusema “tupo tayari kwa lolote” ni ishara kwamba Chama hiki kiliandaa na kujiandaa na fujo zilizotokea”, alisema Nape.

CCM imetoa mwito kwa vyama vya siasa na wanasiasa kwa ujumla kujenga utamaduni wa kuheshimu utawala wa sheria na kusema kwamba amani na utulivu vilivyopo nchini ni kazi nzuri iliyojengwa kwa muda mrefu na waasisi wa taifa la Tanzania kwa kujenga utamaduni wa kuzingatia utawala wa sheria.

Via: Mo Blog
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.

Sunday, September 2, 2012

MSHINDI BSS 2009 PASCAL CASSIAN KUZINDUA ALBAMU YAKE YA INJILI UWANJA WA FISI LEO.


 
Na.Mwandishi Wetu
Mshindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS) 2009 Pascal Cassian atazindua albamu yake ya nyimbo za injili iitwayo Yasamehe Bure leo katika Uwanja wa Fisi.
Albamu hiyo itakayokuwa na nyimbo kama vile Chuki ya Nini, Nikumbuke na Mimi, Jina la Yesu, Mafuriko, Pesa, Baba na Usilie.
Akizungumzia albamu hiyo alisema kuwa ina lenga kuwarudisha waliopotea kwa Mungu kwa kuwapatia ujumbe wa neno la Mungu kwa njia ya nyimbo.
Alisema kuwa akiwa kama kijana ameamua kutumia muda, nguvu na akili zake nyingi katika kumwimbia na kumsifia Mungu na hivyo ameamua kuwafikishia vijana, watoto na watu wazima ujumbe kupitia nyimbo.
Pia akizungumzia sababu ya kuzindulia albam yake katika eneo la uwanja wa Fisi alisema kuwa kutokana na sifa mbaya ya eneo hilo ameamua ambapo limekuwa likifahamika kama uwanja wa dhambi kutokana matukio mbalimbali ambayo yanafanyika mahala hapo.
Alisema kuwa mgeni rasmi anatarajia kuwa Jaji Mkuu wa shindano la Epiq Bongo Star Search (EBSS) Ritha Paulsen ambae ndie alieibua kipaji chake kupitia shindano hilo mwaka 2009 wakati likiitwa BSS.
Uzinduzi huo pia utasindikizwa na waimbaji wengine ambao ni Martha Mwaipaja, Sifa John, Joseph Kaka, Beatrice na wengineo wengi.
Albamu hiyo ambayo ameirekodia katika studio mbalimbali imemchukua miezi mienne kuiandaa na itauzwa kwa shilingi 10000/=.
“ Mimi kwanza ninamshukuru Mungu kwa kuniongoza mpaka kufikia hatua hii ya kuzindua albamu yangu na ameweza kunifikisha hapa kupitia programu ya BSS ambapo ndipo nilionekana uwezo wangu wa kuimba na kushinda na kumbe ilikuwa ndio mwanzo wa safari yangu ya kumtumikia Mungu” alisema Cassian.
MWARICK JAPHET TEKELE MUJUNGU Web Developer

ASANTE KWA KUTEMBELEA KING SELE BLOG KWA MSAADA ZAIDI WASILIANA NASI: E-mail.: mwarickit@gmail.com.